Marko 8

Yesu Alisha Watu 4,000

1 Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia,

2 “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula.

3 Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.”

4 Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?”

5 Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”

Wakajibu, “Tuna mikate saba.”

6 Akawaambia watu waketi chini. Akiisha kuichukua mikate saba na kushukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo.

7 Walikuwa pia na visamaki vichache, Yesu akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu.

8 Wale watu walikula na kutosheka, baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia wakajaza vikapu saba.

9 Watu waliokula walikuwa wapata 4,000. Akiisha kuwaaga,

10 aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake akaenda sehemu za Dalmanutha.

11 Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Yesu. Ili kumtega, wakamwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

12 Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin, nawaambieni, hakitapewa ishara yo yote.”

13 Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ng’ambo.

Chachu Ya Mafarisayo Na Ya Herode

14 Wanafunzi walikuwa wamesahau kuleta mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua.

15 Yesu akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.”

16 Wakaanza kujadiliana wao kwa wao wakasema, “Anasema hivi kwa kuwa hatukuleta mikate.”

17 Yesu akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnazungumzia kuhusu kutokuwa na mikate? Bado hamtambui wala kuelewa? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho?

18 Mna macho lakini mnashindwa kuona, mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki?

19 Nilipoimega ile mikate mitano kuwalisha watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?”

Wakamjibu, “Kumi na viwili.”

20 “Je, nilipomega ile mikate saba kuwalisha watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?”

Wakamjibu, “Saba.”

21 Ndipo akawauliza, “Je, bado tu hamwelewi?”

Yesu Amponya Kipofu Huko Bethsaida

22 Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Yesu amguse.

23 Yesu akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Yesu akamwuliza, “Unaona cho chote?”

24 Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”

25 Yesu akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri.

26 Yesu akamuaga aende nyumbani kwake, akimwambia, “Hata kijijini usiingie.”

Petro Amkiri Yesu Kuwa Ndiye Kristo

27 Yesu na wanafunzi wake wakaondoka kwenda katika vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani Yesu akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”

28 Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya na wengine husema wewe ni mmojawapo wa manabii.”

29 Akawauliza, “Je, ninyi, mnasema mimi ni nani?”

# Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo.”

30 Akawaonya wasimwambie mtu ye yote habari zake.

Yesu Atabiri Juu Ya Kifo Chake

31 Ndipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria na kwamba atauawa na baada ya siku tatu atafufuka.

32 Aliyasema haya waziwazi, ndipo Petro akamchukua kando akaanza kumkemea.

33 Lakini Yesu alipogeuka na kuwaangalia wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, “Rudi nyuma yangu Shetani! Wewe huwazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu.”

34 Ndipo akauita ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.

35 Kwa maana mtu ye yote anayetaka kuiokoa nafsi ataipoteza, lakini yeye ayapotezaye maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa.

36 Mtu atafaidiwa nini kama akiupata ulimwengu wote lakini akaipoteza nafsi yake?

37 Au mtu atatoa nini apate tena maisha yake?

38 Mtu ye yote anayenionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na cha dhambi, Mwana wa Adamu, atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/8-7ce75f79a9969e587597c7701faaa16c.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × five =