Matendo 19

Paulo Huko Efeso

1 Wakati Apolo akiwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa,

2 akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”

Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.”

3 Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.”

4 Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani, Yesu.”

5 Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Yesu.

6 Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri.

7 Idadi yao ilikuwa wapata wanaume kumi na wawili.

8 Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akawa na majadiliano ya kuwafanya watu waamini mambo yanayohusu Ufalme wa Mungu.

9 Lakini baadhi yao kwa ukaidi walipokataa kuamini na kukashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu, Paulo aliachana nao, akawachukua wanafunzi na kuhojiana nao kila siku katika darasa la mtu mmoja aitwaye Tirano.

10 Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko Asia wakawa wamesikia neno la Bwana.

Wana Wa Skewa Wajaribu Kutoa Pepo Mchafu

11 Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo,

12 kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao na pepo wachafu wakawatoka.

13 Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu juu ya wale wenye pepo wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.”

14 Palikuwa na wana saba wa mtu mmoja Myahudi jina lake Skewa, aliyekuwa kiongozi wa makuhani, ambao walikuwa wanafanya hivyo.

15 Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?”

16 Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.

17 Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana.

18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu.

19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakam 50,000za fedha.

20 Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu.

Ghasia Huko Efeso

21 Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.”

22 Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko Asia.

23 Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia ile ya Bwana.

24 Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa,

25 aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii?

26 Pia ninyi mmeona na kusikia jinsi ambavyo si huku Efeso peke yake lakini ni karibu Asia yote huyu Paulo amewashawishi na kuvuta idadi kubwa ya watu kwa kusema kuwa miungu iliyotengenezwa na watu si miungu.

27 Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu mke Artemi, aliye mkuu, anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”

28 Waliposikia maneno haya, wakaghadhabika, wakaanza kupiga kelele, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!”

29 Mara mji wote ukajaa ghasia, wakawakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliokuwa wakisafiri pamoja na Paulo, watu wakakimbilia katika ukumbi wa michezo kama mtu mmoja.

30 Paulo akataka kuingia katikati ya umati wa watu lakini wanafunzi hawakumruhusu.

31 Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi.

32 Baadhi ya watu walikuwa wakilia hivi na wengine vile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko.

33 Wayahudi wakamsukumia Aleksanda mbele na baadhi ya watu kwenye ule umati wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu.

34 Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”

35 Baadaye karani wa mji akaunyamazisha ule umati wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni?

36 Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayakanushiki, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lo lote kwa haraka.

37 Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike.

38 Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana jambo zito dhidi ya mtu ye yote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka.

39 Lakini kama kuna jambo jingine lo lote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali.

40 Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.”

41 Baada ya kusema haya akavunja mkutano.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/19-91ace03528c5a213e2d2c189f40ab9df.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

13 − twelve =