Matendo 21

SAFARI YA TATU YA PAULO YA KITUME

Paulo Aenda Yerusalemu

1 Tulipokwisha kujitenga nao, tukaanza safari kwa njia ya bahari moja kwa moja mpaka Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukaenda Patara.

2 Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo.

3 Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri mpaka Shamu, tukatia nanga katika bandari ya Tiro ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake.

4 Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu.

5 Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba.

6 Baada ya kuagana, tukapanda melini, nao wakarudi majumbani mwao.

7 Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu wanafunzi wa huko tukakaa nao kwa siku moja.

8 Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani kwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale watu saba waliochaguliwa kule Yerusalemu, tukakaa kwake.

9 Filipo alikuwa na binti wanne mabikira ambao walikuwa wanatoa unabii.

10 Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, akatelemka nabii mmoja kutoka Uyahudi jina lake Agabo.

11 Alipotufikia akachukua mshipi wa Paulo akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe akasema, “Roho Mtakatifu anasema: ‘Hivi ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu Mataifa.’ ”

12 Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu.

13 Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.”

14 Alipokuwa hashawishiki, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”

15 Baada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu.

16 Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani kwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.

Paulo Awasili Yerusalemu

17 Tulipofika Yerusalemu ndugu wakatukaribisha kwa furaha.

18 Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulikwenda kumwona Yakobo na wazee wote wa kanisa walikuwepo.

19 Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu Mataifa kwa kupitia huduma yake.

20 Baada ya kusikia mambo haya wakamwadhimisha Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kuna elfu nyingi za Wayahudi walioamini, nao wote wana bidii kwa ajili ya sheria.

21 Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote waishio miongoni mwa watu Mataifa kumkataa Mose na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi.

22 Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu.

23 Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri.

24 Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria.

25 Lakini kuhusu wale watu Mataifa walioamini tumewaandikia uamuzi wetu kwamba wajitenge na kitu cho chote kilichotolewa sadaka kwa sanamu na damu au kula nyama ya mnyama aliyeuawa kwa kunyongwa, tena wajitenge na uasherati.”

26 Ndipo kesho yake Paulo akawachukua wale watu na akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya Hekalu ili akatoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

Paulo Akamatwa

27 Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka sehemu za Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu wakamkamata.

28 Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.”

29 (Walikuwa wamemwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa mjini pamoja na Paulo wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)

30 Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka mle Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa.

31 Walipokuwa wakitaka kumwua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari wa Kirumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko.

32 Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na maaskari wakakimbilia kwenye ile ghasia, wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.

33 Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani na alikuwa amefanya nini.

34 Baadhi ya watu katika ule umati wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine wakisema lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi.

35 Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi maaskari wambebe juu juu kwa sababu fujo za ule umati wa watu zilikuwa kubwa.

36 Ule umati wa watu walikuwa wakifuata wakiendelea kupiga kelele wakisema, “Mwondoe huyu!”

Paulo Anajitetea

37 Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?”

Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani?

38 Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi 4,000 wenye silaha jangwani?”

39 Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso, huko Kilikia, raia wa mji usiokuwa wa kawaida. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”

40 Akiisha kupata ruhusa ya yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza kimya, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema:

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/21-e86edac31bc7014729c50c5db7e652b1.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 + 10 =