Matendo 23

1 Paulo akawakazia macho wale wajumbe wa baraza, akasema, “Ndugu zangu, nimetimiza wajibu wangu kwa Mungu kwa dhamiri safi kabisa hadi leo.”

2 Kwa ajili ya jambo hili Kuhani Mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi kinywani.

3 Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa! Wewe umeketi hapo ili kunihukumu kwa mujibu wa sheria, lakini wewe mwenyewe unakiuka sheria kwa kuamuru kwamba nipigwe kinyume cha sheria!”

4 Wale watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Je, wewe wathubutu kumtukana Kuhani Mkuu wa Mungu?”

5 Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye alikuwa Kuhani Mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usimnenee mabaya kiongozi wa watu wako.’ ”

6 Paulo alipotambua ya kuwa baadhi yao walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo, akapaza sauti kwenye baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana Farisayo. Hapa nimeshtakiwa kuhusu tumaini langu katika ufufuo wa wafu.”

7 Aliposema haya, farakano likaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo na baraza lote likagawanyika.

8 (Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.)

9 Kukawa na ghasia kubwa, nao baadhi ya walimu wa sheria ambao ni Mafarisayo, wakasimama wakapinga kwa nguvu wakisema, “Hatuoni kosa lo lote la mtu huyu! Huenda ikawa roho au malaika amezungumza naye”

10 Ugomvi ukawa mkubwa kiasi kwamba yule jemadari akahofu kuwa wangemrarua Paulo vipande vipande, akaamuru vikosi vya askari vishuke na kumwondoa Paulo katikati yao kwa nguvu na kumleta ndani ya ngome ya jeshi.

11 Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”

Hila Za Kumwua Paulo

12 Kulipopambazuka Wayahudi wakafanya shauri pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo.

13 Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini.

14 Wakawaendea viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejifunga pamoja kwa kiapo kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tumemwua Paulo.

15 Hivyo basi, wewe pamoja na baraza, inawapasa mumjulishe jemadari ili amtelemshe Paulo kwenu, mjifanye kama mnataka kufanya uchunguzi wa kina zaidi wa shauri lake. Nasi tuko tayari kumwua kabla hajafika hapa.”

16 Lakini mtoto wa dada yake Paulo aliposikia juu ya shauri hilo baya, alikwenda kule kwenye ngome ya askari na kumweleza Paulo.

17 Ndipo Paulo akamwita mmoja wa wakuu wa maaskari akamwambia, “Mpeleke huyu kijana kwa jemadari, analo jambo la kumweleza.”

18 Hivyo yule mkuu wa maaskari akampeleka yule kijana kwa jemadari akamwambia, “Paulo, yule mfungwa aliniita na kuniomba nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukueleza.”

19 Yule jemadari akamshika yule kijana mkono, akampeleka kando na kumwuliza, “Unataka kuniambia nini?”

20 Yule kijana akasema, “Wayahudi wamekubaliana wakuombe umpeleke Paulo kwenye baraza lao kesho kwa kisingizio kwamba wanataka kufanya uchunguzi wa kina wa shauri lake.

21 Lakini usishawishiwe nao kwa maana zaidi ya watu arobaini wanamvizia. Wamejifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo. Sasa wako tayari, wanangoja idhini yako kwa ajili ya ombi lao.”

22 Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende na akamwonya, akisema, “Usimwambie mtu ye yote kwamba umenieleza habari hizi.”

Paulo Ahamishiwa Kaisaria

23 Kisha yule jemadari akawaita wakuu wake wawili wa maaskari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari 200, wapanda farasi sabini na watu 200 wenye mikuki.

24 Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mumpeleke salama mpaka kwa mtawala Feliksi.”

25 Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo:

26 Klaudio Lisia,

Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi:

Salamu.

27 Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumwua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya maaskari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raia wa Rumi.

28 Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya baraza lao.

29 Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lo lote linalostahili kifo au kifungo.

30 Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na shauri baya dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara, nikiwaagiza washtaki wake pia waeleze mbele yako mashtaka yao dhidi yake.

31 Hivyo maaskari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta mpaka Antipatri.

32 Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wakati wao walirudi kwenye ngome ya maaskari.

33 Walipofika Kaisaria kumpa mtawala ile barua, walimkabidhi pia Paulo kwake.

34 Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimwuliza Paulo kwamba alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia,

35 alisema, “Nitasikiliza shauri lako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/23-cc3928062fcfec48d02ebcaf63e52ec2.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

5 × five =