Mathayo 11

Yesu Na Yohana Mbatizaji

1 Baada ya Yesu kumaliza kutoa maagizo kwa wale wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

2 Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristoalikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake

3 ili wakamwulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwarifu Yohana yale mnayosikia na kuyaona:

5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema.

6 Ana heri mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

7 Wale wanafunzi wa Yohana walipokuwa wanaondoka, Yesu akaanza kusema na makutano kuhusu Yohana Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipokwenda kule nyikani, mlikwenda kuona nini? Unyasi ukiyumbishwa na upepo?

8 Kama sivyo, mlitoka kwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi mazuri? Hasha, wale wanaovaa nguo nzuri wako katika majumba ya wafalme.

9 Basi mlitoka kwenda kuona nini? Je, ni kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.

10 Huyo ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:

“ ‘Tazama namtuma mjumbe mbele yako,

atakayetengeneza njia mbele yako.’

11 Amin, nawaambia, miongoni mwa watu waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu zaidi ya Yohana Mbatizaji, lakini aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, ni mkuu kuliko Yohana.

12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hadi sasa, Ufalme wa Mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.

13 Kwa maana manabii wote na Torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana.

14 Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye (Yohana) ndiye yule Eliya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja.

15 Yeye aliye na sikio na asikie.

16 “Lakini kizazi hiki nikifananishe na nini? Kinafanana na watoto waliokaa sokoni wakiwaita wenzao na kuwaambia,

17 “ ‘Tuliwapigia filimbi,

lakini hamkucheza;

tuliwaimbia nyimbo za msiba

lakini hamkuomboleza.’

18 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’

19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazama, mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kwa haki ya matendo yake.”

Ole Wa Miji Isiyotubu

20 Ndipo Yesu akaanza kushutumu miji ambamo alifanya miujiza yake mingi kuliko kwingine, kwa maana watu wake hawakutubu.

21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingelifanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu tangu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.

22 Lakini nawaambia, itavumilika zaidi kwa Tiro na Sidoni katika siku ya hukumu, kuliko kwenu.

23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa pande za chini sana. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungalikuwapo hadi leo.

24 Lakini nakuambia kwamba, Sodoma itastahimili zaidi katika siku ile ya hukumu kuliko wewe.”

Hakuna Amjuaye Baba Ila Mwana

25 Wakati huo Yesu alisema, “Ninakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wachanga.

26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na ye yote ambaye Mwana anapenda kumdhihirisha Baba kwake.

Yesu Awaita Waliolemewa Na Mizigo

28 “Njoni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/11-6d29c67c3f89fcc3fabb19fe8888531d.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

fifteen + sixteen =