Mathayo 24

Kubomolewa Kwa Hekalu Kwatabiriwa

1 Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu.

2 Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, amin nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, kila moja litabomolewa.”

Ishara Za Nyakati Za Mwisho

3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia mahali pasipo na watu, wakamwuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nazo ni nini dalili za kuja kwako na za mwisho wa dunia?”

4 Yesu akawajibu, “Angalieni, mtu asiwadanganye.

5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi.

6 Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita, angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.

7 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali.

8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.

9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu.

10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana.

11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi.

12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa,

13 Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ndiye atakayeokoka.

14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni pote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo ule mwisho utakapokuja.

15 “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, asomaye na afahamu,

16 basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani.

17 Ye yote aliyeko juu ya paa la nyumba asishuke ili kuchukua cho chote kutoka ndani ya nyumba.

18 Yeye aliye shambani na asirudi nyumbani kwenda kuchukua vazi lake.

19 Ole wa wenye mimba na wenye watoto wachanga siku hizo!

20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato.

21 Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa, wala haitakuwako tena.

22 Kama siku hizo zisingelifupizwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeliokoka, lakini kwa ajili ya wateule siku hizo zitafupizwa.

23 Wakati huo kama mtu ye yote akiwaambia, ‘Tazama, huyu hapa ni Kristo! Au Kristo yuko kule!’ Msisadiki.

24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo na kufanya ishara kubwa na miujiza mingi ili kuwapotosha, hata ikiwezekana wale wateule hasa.

25 Angalieni, nimetangulia kuwaambia mapema.

26 “Kwa hiyo mtu ye yote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki.

27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

28 Kwa maana po pote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.

Kuja Kwa Mwana Wa Adamu

29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile,

“ ‘jua litatiwa giza,

nao mwezi hautatoa nuru yake;

nazo nyota zitaanguka kutoka angani,

na nguvu za anga zitatikisika.’

30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu.

31 Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.

32 “Jifunzeni kutokana na mtini. Matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchipua majani, fahamuni kwamba kiangazi kimekaribia.

33 Hata hivyo, mwonapo mambo hayo, jueni kwamba yu karibu malangoni.

34 Amin, amin nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.

35 Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Hakuna Ajuaye Siku Wala Saa

36 “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna ajuaye, hata malaika mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.

37 Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

38 Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia kwenye safina,

39 nao hawakujua lo lote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu.

40 Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mwingine ataachwa.

41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja, mmoja atatwaliwa, mwingine ataachwa.

42 “Kwa hiyo kesheni, kwa maana hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu.

43 Lakini fahamuni hili kwamba: Kama mwenye nyumba angelijua ni wakati gani wa usiku ambao mwivi anakuja, angelikesha na asingeliiacha nyumba yake kuvunjwa.

44 Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.

Mfano Wa Mtumishi Mwaminifu

45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati muafaka?

46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo.

47 Amin, amin nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote.

48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’

49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake na kula na kunywa pamoja na walevi,

50 bwana wa mtumishi huyo atakuja siku ambayo mtumishi huyo hamtazamii na saa ile ambayo haijui.

51 Atamkata huyo mtumishi vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/24-12b492eae209243b33cb8e7d8107616c.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

sixteen − 9 =