Mathayo 27

Yesu Aletwa Mbele Ya Pilato

1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumwua.

2 Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala.

Yuda Ajinyonga

3 Yuda, ambaye ndiye aliyekuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.

4 Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”

Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”

5 Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.

6 Wale makuhani wakuu wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.”

7 Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni.

8 Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo.

9 Ndipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli,

10 wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”

Yesu Mbele Ya Pilato

11 Wakati Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamwuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.”

12 Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno.

13 Ndipo Pilato akamwuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?”

14 Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.

15 Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja atakayechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu.

16 Wakati huo alikuwapo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba.

17 Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?”

18 Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.

19 Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lo lote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”

20 Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.

21 Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”

Wakajibu, “Baraba.”

22 Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?”

Wakajibu wote, “Msulibishe!”

23 Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”

Lakini wao wakazidi kupiga kelele, “Msulibishe.”

24 Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lo lote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”

25 Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”

26 Basi akawafungulia Baraba na baada ya kumchapa Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe.

Askari Wamdhihaki Yesu

27 Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitoriona wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka.

28 Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha

29 wakasokota taji ya miiba wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki wakisema “salamu, mfalme wa Wayahudi!”

30 Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena.

31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile vazi, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili kumsulibisha.

Yesu Asulibishwa

32 Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.

33 Wakafika mahali paitwapo Golgotha (ambayo maana yake ni, Mahali pa Fuvu la Kichwa),

34 wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe, lakini alipoionja, akakataa kuinywa.

35 Walipokwisha kumsulibisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura, [ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”]

36 Kisha wakaketi, wakamchunga.

37 Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake: HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI.

38 Wanyang’anyi wawili walisulibiwa pamoja naye, mmoja kuume kwake na mwingine kushoto kwake.

39 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamvurumishia matukano huku wakitikisa vichwa vyao

40 na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.”

41 Vivyo hivyo, viongozi wa, makuhani, walimu wa sheria na wazee wakamdhihaki wakisema,

42 “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, tutamwamini.

43 Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ”

44 Hata wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.

Kifo Cha Yesu

45 Tangu saa sita hadi saa tisa giza lilifunika nchi yote.

46 Ilipofika saa tisa Yesu akapaza sauti akalia,“Eloi, Eloi lama Sabakthani?”Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

47 Baadhi ya wale watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia haya, wakasema “Anamwita Eliya.”

48 Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi akampa Yesu ili anywe.

49 Wengine wakasema, “Mwacheni na tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.”

50 Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.

51 Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka.

52 Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuka.

53 Wakatoka makaburini na baada ya Yesu kufufuka waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.

54 Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, wakaogopa wakasema, “Hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu!”

55 Walikuwako wanawake huko, wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulika na mahitaji yake.

56 Miongoni mwao walikuwapo Maria Magdalene, Maria mama yake Yakobo na Yosefu na mama yao wana wa Zebedayo.

Maziko Ya Yesu

57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathea aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.

58 Akamwendea Pilato, kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe.

59 Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akauviringishia nguo ya kitani safi nyeupe

60 na kuuzika kwenye kaburi lake mwenyewe jipya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mlangoni mwa kaburi, akaenda zake.

61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwapo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.

Walinzi Pale Kaburini

62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato

63 na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu kabla hajafa alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’

64 Kwa hiyo uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti mpaka baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuka kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”

65 Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadri mwezavyo.”

66 Kwa hiyo wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/27-52f4057a249835fb52788d246254f4bf.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × 3 =