Mhubiri 10

1 Kama vile mainzi waliokufa huacha harufu mbaya kwenye manukato,

ndivyo upumbavu kidogo huzidi nguvu hekima na heshima.

2 Moyo wa mwenye hekima huelekea kuume,

lakini moyo wa mpumbavu huelekea kushoto.

3 Hata anapotembea barabarani,

mpumbavu hukosa ufahamu

na kudhihirisha kwa kila mmoja

jinsi alivyo mpumbavu.

4 Kama hasira ya mtawala ikiwaka dhidi yako,

usiache mahali pako,

utulivu huweza kuzuia makosa mengi.

5 Kuna ubaya niliouona chini ya jua,

aina ya kosa litokalo kwa mtawala:

6 Wapumbavu kuwekwa kwenye nafasi nyingi za juu,

wakati matajiri hushika nafasi za chini.

7 Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi,

wakati wakuu wakitembea

kwa miguu kama watumwa.

8 Yeye achimbaye shimo

aweza kutumbukia ndani yake,

ye yote abomoaye ukuta

anaweza kuumwa na nyoka.

9 Ye yote apasuaye mawe

inawezekana yakamuumiza,

ye yote apasuaye magogo

inawezekana yakamuumiza.

10 Kama shoka ni butu

na halikunolewa,

nguvu nyingi zinahitajika,

lakini ustadi utaleta mafanikio.

11 Kama nyoka akiuma kabla ya kufanyiwa uaguzi,

mwaguzi hatahitajika tena.

12 Maneno yatokayo kinywani mwa mtu mwenye hekima

yana neema,

bali mpumbavu huangamizwa

na midomo yake mwenyewe.

13 Mwanzoni maneno yake ni upumbavu,

mwishoni ni wazimu mbaya,

14 naye mpumbavu huzidisha maneno.

Hakuna ye yote ajuaye linalokuja,

ni nani awezaye kueleza ni jambo gani

litakalotokea baada yake?

15 Kazi ya mpumbavu humchosha mwenyewe,

hajui njia iendayo mjini.

16 Ole wako, Ee nchi ambayo mfalme wako alikuwa mtumwa

na ambayo wakuu wako hufanya karamu asubuhi.

17 Heri wewe, Ee nchi ambayo mfalme wako ni wa uzao wenye kuheshimika

na ambayo wakuu wako hula chakula kwa wakati unaofaa:

ili kupata nguvu na si kwa ajili ya ulevi.

18 Kama mtu ni mvivu paa la nyumba huinama,

kutokana na mikono milegevu, nyumba huvuja.

19 Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko,

nao mvinyo hufurahisha maisha,

lakini fedha ni jawabu la mambo yote.

20 Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako,

au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala,

kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako,

naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ECC/10-5fbbca5ca6a26cbbf73b2867d8138052.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 × 2 =