Mithali 11

1 Bwanahuchukia sana mizani za udanganyifu,

bali vipimo sahihi ni furaha yake.

2 Kiburi kinapokuja, ndipo huja aibu,

bali unyenyekevu huja na hekima.

3 Uadilifu wa wenye haki huwaongoza,

bali wasio waaminifu huharibiwa na hila yao.

4 Utajiri haufaidii kitu katika siku ya ghadhabu,

bali haki huokoa kutoka mautini.

5 Haki ya wasio na lawama, huwatengenezea njia iliyonyooka,

bali waovu huangushwa kwa uovu wao wenyewe.

6 Haki ya wanyofu huwaokoa,

bali wasio waaminifu hunaswa na tamaa mbaya.

7 Wakati mtu mwovu anapokufa, matumaini yake hutoweka,

yote aliyoyatazamia kutokana na nguvu zake huwa si kitu.

8 Mtu mwenye haki huokolewa kutoka katika taabu,

naye mtu mwovu huingia humo badala yake.

9 Kwa kinywa chake mtu asiyemwamini Mungu

humwangamiza jirani yake,

bali kwa maarifa mwenye haki huokolewa.

10 Wakati mwenye haki anapofanikiwa, mji hufurahi,

mwovu atowekapo, huwa kuna kelele za furaha.

11 Kutokana na baraka ya mtu mnyofu mji hukwezwa,

bali kwa kinywa cha mwovu mji huharibiwa.

12 Mtu asiye na akili humdharau jirani yake,

bali mtu mwenye ufahamu huuzuia ulimi wake.

13 Masengenyo husaliti tumaini,

bali mtu mwaminifu hutunza siri.

14 Pasipo ushauri wa hekima taifa huanguka,

bali washauri wengi hufanya ushindi uwe wa hakika.

15 Yeye amdhaminiye mgeni hakika atateseka,

bali ye yote akataaye kuunga mkono dhamana ni salama.

16 Mwanamke mwenye moyo wa huruma hupata heshima,

bali wanaume wakorofi hupata mali tu.

17 Mwanaume mwenye huruma hujinufaisha mwenyewe,

bali mwanaume katili hujiletea taabu mwenyewe.

18 Mtu mwovu hupata ujira wa udanganyifu,

bali yeye apandaye haki huvuna tuzo ya uhakika.

19 Mtu mwenye haki kweli kweli hupata uzima,

bali yeye afuatiliaye ubaya huendea kifo chake.

20 Bwanahuwachukia sana watu wenye moyo wa upotovu,

bali hupendezwa na wale ambao njia zao hazina lawama.

21 Uwe na hakika na hili: Waovu hawataepuka kuadhibiwa,

bali wale wenye haki watakuwa huru.

22 Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe

ndivyo alivyo mwanamke mzuri ambaye hana busara.

23 Shauku ya mwenye haki huishia tu kwenye mema,

bali tumaini la mwovu huishia tu kwenye ghadhabu.

24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,

mwingine huzuia, lakini huwa maskini.

25 Mtu mkarimu atastawi;

yeye awaburudishaye wengine

ataburudishwa mwenyewe.

26 Watu humlaani mtu awanyimae watu nafaka,

bali baraka itamkalia kichwani kama taji

yeye aliye radhi kuiuza.

27 Yeye atafutaye mema hupata ukarimu,

bali ubaya huja kwake yeye autafutaye.

28 Ye yote ategemeaye utajiri wake ataanguka,

bali mwenye haki atastawi kama jani bichi.

29 Yeye aletaye taabu kwa jamaa yake atarithi tu upepo,

naye mpumbavu atakuwa mtumishi wa wenye hekima.

30 Tunda la mwenye haki ni mti wa uzima,

naye mwenye hekima huvuta roho za watu.

31 Kama wenye haki watapokea ujira wao duniani,

si zaidi sana wasiomcha Mungu na wenye dhambi!

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/11-81584545fab6ddaa41d75fc3209ba4c1.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

17 − 4 =