Mithali 30

Mithali Za Aguri

1 Mithali za Aguri mwana wa Yake, mausia:

Huyu mtu alimwambia Ithieli,

naam, Ithieli na Ukali:

2 “Mimi ni mjinga kuliko wanadamu wote;

sina ufahamu wa kibinadamu.

3 Sijajifunza hekima,

wala sina maarifa ya kumjua yeye Aliye Mtakatifu.

4 Ni nani ameshapanda mbinguni na kushuka?

Ni nani ameshakusanya upepo

kwenye vitanga vya mikono yake?

Ni nani ameshafungia maji kwenye nguo yake?

Ni nani ameimarisha miisho yote ya dunia?

Jina lake ni nani na mwanawe anaitwa nani?

Niambie kama unajua!

5 “Kila neno la Mungu ni kamilifu;

yeye ni ngao kwa wale wanaomkimbilia.

6 Usiongeze kwenye maneno yake,

ama atakukemea na kukuthibitisha kuwa mwongo.

7 “Ninakuomba vitu viwili, EeBwana;

usininyime kabla sijafa:

8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;

usinipe umaskini wala utajiri,

bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.

9 Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana

na kusema, ‘Bwanani nani?’

Au nisije nikawa maskini nikaiba,

nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.

10 “Usimchongee mtumishi kwa bwana wake,

asije akakulaani, ukapatilizwa kwalo.

11 “Wako watu wale ambao huwalaani baba zao

na wala hawawabariki mama zao;

12 wale ambao ni safi machoni pao wenyewe

kumbe hawakuoshwa uchafu wao;

13 wale ambao daima macho yao ni ya kiburi,

ambao kutazama kwao ni kwa dharau;

14 wale ambao meno yao ni panga

na ambao mataya yao yamewekwa visu

kuwaangamiza maskini katika nchi,

na wahitaji kutoka miongoni mwa wanadamu.

15 “Mruba anao binti wawili waliao,

‘Nipe! Nipe!’

“Kuna vitu vitatu visivyotosheka kamwe,

naam, viko vinne visivyosema, ‘Yatosha!’:

16 Ni kaburi, tumbo lisilozaa,

nchi, isiyoshiba maji kamwe,

na moto, usiosema kamwe, ‘Yatosha!’

17 “Jicho lile limdhihakilo baba,

lile linalodharau kumtii mama,

litang’olewa na kunguru wa bondeni,

litaliwa na tai.

18 “Kuna vitu vitatu vinavyonishangaza sana,

naam, vinne nisivyovielewa:

19 Ni mwendo wa tai katika anga,

mwendo wa nyoka juu ya mwamba,

mwendo wa meli katika maji makuu ya bahari,

nao mwendo wa mtu pamoja na msichana.

20 “Huu ndio mwendo wa mwanamke mzinzi,

hula akapangusa kinywa chake na kusema,

‘Sikufanya cho chote kibaya.’

21 “Kwa mambo matatu nchi hutetemeka,

naam, kwa mambo manne haiwezi kuvumilia:

22 Mtumwa awapo mfalme,

mpumbavu ashibapo chakula,

23 mwanamke asiyependwa aolewapo,

naye mtumishi wa kike achukuapo nafasi ya bibi yake.

24 “Vitu vinne duniani vilivyo vidogo,

lakini vina akili nyingi sana:

25 Mchwa ni viumbe wenye nguvu ndogo,

hata hivyo hujiwekea akiba ya chakula chao wakati wa kiangazi.

26 Pelele ni viumbe vyenye uwezo mdogo

hata hivyo hujitengenezea nyumba zao kwenye miamba.

27 Nzige hawana mfalme,

hata hivyo huenda pamoja vikosi vikosi.

28 Mjusi anaweza kushikwa kwa mkono,

hata hivyo huonekana katika majumba ya kifalme.

29 “Viko vitu vitatu ambavyo vinapendeza katika mwendo wao,

naam, vinne ambavyo hutembea kwa mwendo wa madaha:

30 simba, mwenye nguvu miongoni mwa wanyama,

asiyerudi nyuma kwa cho chote;

31 jogoo atembeaye kwa maringo, pia beberu,

naye mfalme pamoja na jeshi lake lililomzunguka.

32 “Ikiwa umefanya upumbavu na ukajitukuza mwenyewe,

au kama umepanga mabaya,

piga kinywa chako kofi.

33 Kwa maana kama vile kusukasuka maziwa hutoa siagi,

na pia kule kufinya pua hutoa damu,

kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/30-15e152ecb99384ffbe2c5150455bf405.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

8 + nine =