Mithali 8

Wito Wa Hekima

1 Je, hekima haiti?

Je, ufahamu hapazi sauti?

2 Juu ya miinuko karibu na njia,

penye njia panda, ndipo asimamapo,

3 kando ya malango yaelekeayo mjini,

kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema:

4 “Ni ninyi wanaume, ninaowaita,

ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote.

5 Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili,

ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu.

6 Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema,

ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa.

7 Kinywa changu husema lililo kweli,

kwa maana midomo yangu huchukia uovu.

8 Maneno yote ya kinywa changu ni haki,

hakuna mojawapo lililopotoka wala ukaidi.

9 Kwa wenye kupambanua yote ni sahihi,

hayana kasoro kwa wale wenye maarifa.

10 Chagua mafundisho yangu badala ya fedha,

maarifa badala ya dhahabu safi,

11 kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani

na hakuna cho chote unachohitaji kinacholingana naye.

12 “Mimi hekima, nakaa pamoja na busara,

ninamiliki maarifa na busara.

13 KumchaBwanani kuchukia uovu,

ninachukia kiburi na majivuno,

tabia mbaya na mazungumzo potovu.

14 Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu,

nina ufahamu na nina nguvu.

15 Kwa msaada wangu wafalme hutawala

na watawala hutunga sheria zilizo za haki,

16 kwa msaada wangu wakuu hutawala,

na wenye vyeo wote watawalao dunia.

17 Nawapenda wale wanipendao,

na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.

18 Utajiri na heshima viko kwangu,

utajiri udumuo na mafanikio.

19 Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi,

kile nitoacho hupita fedha iliyo bora.

20 Natembea katika njia ya unyofu

katika mapito ya haki,

21 nawapa utajiri wale wanipendao

na kuzijaza hazina zao.

22 “Bwanaaliniumba mwanzoni mwa kazi yake,

kabla ya matendo yake ya zamani;

23 niliteuliwa tangu milele,

tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa.

24 Wakati hazijakuwapo bahari, nilikwishazaliwa,

wakati hazijakuwapo chemchemi zilizojaa maji,

25 kabla milima haijawekwa mahali pake,

kabla vilima havijakuwapo, nilikwishazaliwa,

26 kabla hajaumba dunia wala mashamba yake

au vumbi lo lote la dunia.

27 Nilikuwapo alipoziweka mbingu mahali pake,

wakati alipochora mstari wa upeo wa macho

juu ya uso wa kilindi,

28 wakati alipoweka mawingu juu

na kuziweka imara chemchemi za bahari,

29 wakati alipoiwekea bahari mpaka wake

ili maji yasivunje agizo lake,

na wakati alipoweka misingi ya dunia.

30 Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake.

Nilijazwa na furaha siku baada ya siku,

nikifurahi daima mbele zake,

31 nikifurahi katika dunia yake yote

nami nikiwafurahia wanadamu.

32 “Basi sasa wanangu, nisikilizeni;

heri wale wanaozishika njia zangu.

33 Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima;

msiyapuuze.

34 Heri mtu yule anisikilizae mimi,

akisubiri siku zote malangoni mwangu,

akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu.

35 Kwa maana ye yote anipatae mimi amepata uzima

na kujipatia kibali kutoka kwaBwana.

36 Lakini ye yote ashindwaye kunipata

hujiumiza mwenyewe;

na wote wanichukiao mimi hupenda mauti.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/8-d4c99cb9aea433eb7256382a216b2dca.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

six + 15 =