Ufunuo 12

Mwanamke Na Joka

1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua na mwezi ukiwa chini ya miguu yake na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake.

2 Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa.

3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake.

4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa.

5 Yule mwanamke akazaa mtoto mwanamume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi.

6 Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.

Malaika Mikaeli Amshinda Yule Joka

7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao.

8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa na hapakuwa tena na nafasi kwa ajili yao mbinguni.

9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwenguni wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

Ushindi Mbinguni Watangazwa

10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema:

“Sasa Wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja

na mamlaka ya Kristo wake.

Kwa kuwa ametupwa chini

mshtaki wa ndugu zetu,

anayewashtaki mbele za Mungu

usiku na mchana.

11 Nao wakamshinda

kwa damu ya Mwana-Kondoo

na kwa neno la ushuhuda wao.

Wala wao hawakuyapenda maisha yao

hata kufa.

12 Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu

na wote wakaao humo!

Lakini ole wenu nchi na bahari,

kwa maana huyo Shetani ameshuka kwenu,

akiwa amejaa ghadhabu,

kwa sababu anajua ya kuwa

muda wake ni mfupi!”

13 Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto mwanamume.

14 Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka mpaka mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko nyikani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu, wakati ambako yule joka hawezi kufika.

15 Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke na kumkumba kama mafuriko.

16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao huyo joka alikuwa ameutoa kinywani mwake.

17 Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke, likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo. Lile joka likasimama kwenye mchanga wa bahari.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/12-ac1302b27797bf067ba61a0c115d7adf.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

one × two =