Ufunuo 15

Malaika Saba Na Mapigo Saba

1 Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni, malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika.

2 Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu.

3 Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu na wimbo wa Mwana-Kondoo wakisema:

“BWANA Mungu Mwenyezi,

matendo yako ni makuu na ya ajabu.

Njia zako wewe ni za haki na za kweli

Mfalme wa nyakati zote!

4 Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana

na kulitukuza jina lako?

Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu.

Mataifa yote yatakuja

na kuabudu mbele zako,

kwa kuwa matendo yako ya haki

yamedhihirishwa.”

5 Baada ya haya nikatazama, nalo Hekalu la hema la Ushuhuda lilikuwa limefunguliwa mbinguni.

6 Ndani ya lile Hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani ing’aayo na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao.

7 Ndipo mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele.

8 Nalo lile Hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna ye yote aliyeweza kuingia mle Hekaluni mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/15-3ec0b7ac9fb05e65ff21005342ee7cc5.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ten − four =