Ufunuo 18

Kuanguka Kwa Babeli

1 Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu na dunia ikamulikiwa na mng’ao wake.

2 Naye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema:

“Umeanguka! Umeanguka Babeli uliye Mkuu!

Umekuwa makao ya mashetani

na makazi ya kila pepo mchafu,

makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye.

3 Kwa maana mataifa yote yamekunywa

mvinyo wa uasherati wake.

Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye,

nao wafanya biashara wa dunia

wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”

4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema:

“Tokeni katikati yake, enyi watu wangu,

ili msije mkashiriki dhambi zake,

ili msije mkapatwa na pigo lake lo lote;

5 kwa kuwa dhambi zake zimerundikana hadi mbinguni,

naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake.

6 Mtendee kama yeye alivyotenda;

umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda.

Katika kikombe chake mchanganyie

mara mbili ya kile alichochanganya.

7 Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na

utukufu na anasa alizojipatia.

Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema,

‘Mimi ninatawala kama malkia;

mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’

8 Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja:

mauti, maombolezo na njaa.

Naye atateketezwa kwa moto,

kwa maana amhukumuye

ni BWANA Mungu Mwenyezi.

9 “Wafalme wa dunia waliozini naye na kushiriki anasa zake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watamlilia na kumwombolezea.

10 Watasimama mbali na kulia kwa hofu kutokana na mateso yake na kusema:

“ ‘Ole! Ole Ee mji mkubwa,

Ee Babeli mji wenye nguvu!

Hukumu yako imekuja katika saa moja!’

11 “Wafanyabiashara wa dunia watalia na kuomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena:

12 Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya manukato, vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba nyeusi, chuma na marmar,

13 mdalasini, vikolezi, uvumba, manemane, uvumba wenye harufu nzuri, divai, mafuta ya zeituni, unga mzuri na ngano, ng’ombe na kondoo, farasi na magari, watumwa, pia na roho za wanadamu.

14 “Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’

15 Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza wakipiga kelele wakisema:

16 “ ‘Ole! Ole, Ee, mji mkubwa,

uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi,

ya rangi ya zambarau na nyekundu,

ukimetameta kwa dhahabu,

vito vya thamani na lulu!

17 Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa

kama huu umeangamia!’

“Kila nahodha, mabaharia wote wasafirio baharini na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali naye.

18 Watakapoona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’

19 Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema:

“ ‘Ole! Ole, Ee mji mkubwa,

mji ambao wote wenye meli baharini

walitajirika kwa kupitia mali zake!

Katika saa moja tu ameangamizwa!

20 Furahia kwa ajili yake, Ee mbingu!

Furahini watakatifu, mitume na manabii!

Kwa kuwa Mungu amemhukumu

kwa vile alivyowatendea ninyi.’ ”

21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia akalitupa baharini akisema:

“Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli

utakavyotupwa chini kwa nguvu

wala hautaonekana tena.

22 Nyimbo za wapiga vinubi na waimbaji,

wapiga filimbi na sauti za wapiga tarumbeta

kamwe hazitasikika tena ndani yako.

Ndani yako kamwe hataonekana tena fundi

mwenye ujuzi wa aina yo yote.

Wala sauti ya jiwe la kusagia

kamwe haitasikika tena.

23 Mwanga wa taa

hautaangaza ndani yako tena.

Sauti ya bwana arusi na bibi arusi

kamwe haitasikiwa ndani yako tena.

Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia.

Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako.

24 Ndani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu

na wote waliouawa duniani.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/18-5c6f9d4423132dd19237fa2f94162b51.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eleven + twenty =