Ufunuo 7

Waisraeli 144,000 Watiwa Muhuri

1 Baada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili kwamba pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wo wote.

2 Nikaona malaika mwingine akipanda kutoka maawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema,

3 “Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye vipaji vya nyuso za watumishi wa Mungu wetu.”

4 Ndipo nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: yaani 144,000 kutoka katika makabila yote ya Israeli.

5 Kutoka kabila la Yuda 12,000,

kabila la Reubeni 12,000,

kabila la Gadi 12,000,

6 kabila la Asheri 12,000,

kabila la Naftali 12,000,

kabila la Manase 12,000,

7 kabila la Simeoni 12,000,

kabila la Lawi 12,000,

kabila la Isakari 12,000,

8 kabila la Zabuloni 12,000,

kabila la Yosefu 12,000,

na kabila la Benyamini 12,000.

Umati Mkubwa Wa Watu Kutoka Mataifa Yote

9 Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna ye yote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao.

10 Nao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema:

“Wokovu una Mungu wetu,

yeye aketiye kwenye kiti cha enzi

na Mwana-Kondoo!”

11 Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu,

12 wakisema:

“Amen!

Sifa na utukufu

na hekima na shukrani na heshima

na uweza na nguvu

viwe kwa Mungu wetu milele na milele.

Amen!”

13 Kisha mmoja wa wale wazee ishirini na wanne akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”

14 Nikamjibu, “Bwana, wewe wajua.”

Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa.

15 Kwa hiyo,

“Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu

na kumtumikia usiku na mchana

katika Hekalu lake;

naye aketiye katika kile kiti cha enzi

atakaa pamoja nao na kuwalinda.

16 Kamwe hawataona njaa

wala kiu tena.

Jua halitawapiga

wala joto lo lote liunguzalo.

17 Kwa maana Mwana-Kondoo

aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi

atakuwa Mchungaji wao;

naye atawaongoza kwenda

kwenye chemchemi za maji yaliyo hai.

Naye Mungu atafuta kila chozi

kutoka katika macho yao.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/7-8b7013eb05bcff29f19be4256b6999e8.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 − two =