Waamuzi 11

1 Basi Yefta Mgileadi alikuwa mtu shujaa. Baba yake alikuwa Gileadi, naye mama yake alikuwa kahaba.

2 Mke wa Gileadi akamzalia wana wengine, nao watoto hao walipokua, wakamfukuza Yefta na kumwambia, “Wewe huwezi kupata urithi katika jamaa yetu, kwa sababu wewe ni mwana wa mwanamke mwingine.”

3 Basi Yefta akawakimbia ndugu zake akaenda kuishi katika nchi ya Tobu, mahali ambako watu waasi walijiunga naye na kumfuata.

4 Baada ya muda Waamoni wakafanya vita na Israeli,

5 viongozi wa Gileadi wakaenda kumchukua Yefta katika nchi ya Tobu.

6 Wakamwambia Yefta, “Uwe jemadari wetu, ili tuweze kupigana na Waamoni.”

7 Yefta akawaambia, “Je, hamkunichukia mimi na kunifukuza katika nyumba ya baba yangu? Kwa nini mnanijia sasa, wakati mna matatizo.”

8 Viongozi wa Gileadi wakamwambia, “Lakini sasa tumegeuka kukuelekea wewe, ili uende pamoja nasi kupigana na Waamoni, nawe utakuwa kiongozi wetu juu ya watu wote wa Gileadi.”

9 Yefta akawaambia, “Ikiwa mtanirudisha kwetu kupigana na Waamoni, nayeBwanaakanisaidia kuwashinda, Je, ni kweli nitakuwa kiongozi wenu?”

10 Viongozi wa Gileadi wakamjibu, “Bwanandiye shahidi yetu, kwa hakika tutafanya kama usemavyo.”

11 Basi Yefta akaenda na viongozi wa Gileadi, nao watu wakamfanya kiongozi na jemadari wao. Naye akarudia maneno yake yote mbele zaBwanahuko Mizpa.

12 Ndipo Yefta akatuma wajumbe kwa mfalme wa Waamoni akisema, “Una nini juu yetu, hata umekuja kushambulia nchi yetu?”

13 Mfalme wa Waamoni akawajibu wajumbe wale wa Yefta, “Wakati Waisraeli walipopanda kutoka Misri, waliichukua nchi yangu kuanzia Arnoni mpaka Yaboki, hadi kufikia Yordani. Sasa rudisha kwa amani.”

14 Yefta akarudisha wajumbe kwa mfalme wa Waamoni,

15 kusema:

“Hili ndilo asemalo Yefta, Israeli hawakuchukua nchi ya Moabu wala ya Waamoni.

16 Lakini walipopanda kutoka Misri, Israeli walipitia katika jangwa hadi Bahari ya Shamu na wakafika Kadeshi.

17 Ndipo Israeli wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu, wakisema, ‘Tupe ruhusa kupita katika nchi yako,’ Lakini mfalme wa Edomu hakutusikia. Wakapeleka pia wajumbe kwa mfalme wa Moabu, naye akakataa. Kwa hiyo Israeli wakakaa huko Kadeshi.

18 “Baadaye wakasafiri kupitia katika jangwa wakiambaa-ambaa na hiyo nchi ya Edomu na Moabu, wakapitia upande wa mashariki wa nchi ya Moabu na kupiga kambi upande mwingine wa Arnoni. Hawakuingia katika nchi ya Moabu kwa kuwa Arnoni ilikuwa ndio mpaka wake.

19 “Kisha Israeli wakatuma wajumbe kwa Sihoni mfalme wa Waamoni, aliyetawala Heshboni, na kumwambia, ‘Tupe ruhusa kupita katika nchi yako ili kufikia mahali petu.’

20 Hata hivyo, Sihoni hakuwaamini Waisraeli kupita katika nchi yake. Akaandaa jeshi lake lote na kupiga kambi huko Yahasa, nao wakapigana na Israeli.

21 “NdipoBwana, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawashinda. Israeli wakaitwaa nchi yote ya Waamoni, waliokuwa wakiishi katika nchi hiyo,

22 wakiiteka nchi yote kuanzia Arnoni mpaka Yaboki na kutoka jangwani mpaka Yordani.

23 “Basi kwa kuwaBwana, Mungu wa Israeli, amewafukuza Waamoni watoke mbele ya watu wake Israeli, wewe unayo haki gani ya kuitamalaki?

24 Je, haikupasi kuchukua kile ambacho mungu wako Kemoshi amekupa? Vivyo hivyo, cho chote kileBwanaMungu wetu alichotupa sisi, tutakimiliki.

25 Je, wewe ni bora kuliko Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu? Je, yeye alishagombana na Israeli au kupigana nao wakati wo wote?

26 Kwa maana kwa miaka 300 Israeli wameishi Heshboni na vijiji vyake, Aroeri na vijiji vyake, na katika miji yote iliyo kando ya Arnoni. Kwa nini wewe haukuichukua wakati huo?

27 Mimi sijakukosea jambo lo lote, bali wewe ndiye unayenikosea kwa kufanya vita nami. BasiBwana, aliye Mwamuzi, leo na aamue ugomvi kati ya Waisraeli na Waamoni.”

28 Hata hivyo, Mfalme wa Waamoni, hakuyajali maneno ya ujumbe wa Yefta.

29 Ndipo Roho waBwanaakaja juu ya Yefta. Akapita katikati ya Gileadi na Manase, pia akapita katika Mizpa ya Gileadi, na kutokea huko akasonga mbele kushambulia Waamoni.

30 Naye Yefta akaweka nadhiri mbele zaBwanaakisema, “Ikiwa utawatia Waamoni mikononi mwangu,

31 cho chote kile kitakachotoka katika mlango wa nyumba yangu cha kwanza ili kunilaki nirudipo kwa amani katika kuwashinda Waamoni, kitakuwa ni chaBwanana nitakitoa kuwa sadaka ya kuteketezwa.”

32 Ndipo Yefta akavuka kupigana na hao Waamoni, nayeBwanaakawatia mkononi mwake.

33 Akawapiga kwa ushindi mkubwa kuanzia Aroeri mpaka karibu na Minithi na kuendelea mpaka Abel-Keramimu, miji yote iliyopigwa ni ishirini. Basi Israeli wakawashinda Waamoni.

34 Yefta aliporudi nyumbani Mizpa, tazama, binti yake akatoka ili kumlaki kwa matari na kucheza. Alikuwa ndiye mtoto pekee, hakuwa na mwana wala binti mwingine.

35 Alipomwona akararua mavazi yake akalia, “Ee! Binti yangu! Umenifanya niwe na huzuni na kunyong’onyea sana, kwa kuwa nimeweka nadhiri kwaBwana, ambayo siwezi kuivunja.”

36 Akajibu, “Baba yangu, umetoa neno lako kwaBwana. Nitendee mimi kama vile ulivyoahidi, kwa kuwaBwanaamekupatia ushindi dhidi ya adui zako Waamoni.”

37 Naye akamwambia baba yake, “Naomba nifanyiwe jambo hili. Mimi na nipewe miezi miwili ili kuzunguka vilimani nikaulilie ubikira wangu, mimi na wenzangu.”

38 Baba yake akamwambia, “Waweza kwenda.” Naye akamwacha aende kwa miezi miwili. Hivyo akaondoka pamoja na wasichana wenzake, naye akaulilia ubikira wake huko vilimani kwa sababu asingeolewa kamwe.

39 Baada ya hiyo miezi miwili, alirejea kwa baba yake, naye baba yake akamtendea kama alivyokuwa ametoa nadhiri yake. Naye alikuwa bikira.

Nayo ikawa desturi katika Israeli,

40 kwamba kila mwaka binti za Israeli huenda kwa siku nne ili kumkumbuka huyo binti wa Yefta, Mgileadi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JDG/11-947eb34a84206439b4e00dded81c0313.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

9 − six =