Waebrania 11

Maana Ya Imani

1 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni udhahiri wa mambo yasiyoonekana.

2 Naam, kwa imani baba zetu wa kale walishuhudiwa.

3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana viliumbwa kwa vitu visivyoonekana.

Mfano Wa Abeli, Enoki Na Noa

4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.

5 Kwa imani Enoki alitwaliwa kutoka katika maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu.

6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana ye yote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.

7 Kwa imani, Noa alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.

Imani Ya Abrahamu

8 Kwa imani Abrahamu, alipoitwa aende mahali ambapo Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakokwenda.

9 Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni, akaishi katika mahema, kama Isaki na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

10 Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

11 Kwa imani Abrahamu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angelitimiza ahadi yake.

12 Hivyo kutokana na huyu huyu ambaye alikuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.

13 Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani.

14 Watu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe.

15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko.

16 Lakini badala yake wanatamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.

17 Kwa imani Abrahamu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaki kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu.

18 Ingawa Mungu alikuwa amemwambia Abrahamu, “Uzao wako utahesabiwa kwa njia ya Isaki,”

19 Abrahamu alihesabu kuwa Mungu angaliweza kumfufua Isaki kutoka kwa wafu na kwa kusema kwa mfano alimpata tena Isaki kutoka kwa wafu.

20 Kwa imani Isaki alimbariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye.

21 Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.

22 Kwa imani, Yosefu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa wana wa Israeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake.

Imani Ya Mose

23 Kwa imani, wazazi wa Mose walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

24 Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao.

25 Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu.

26 Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye.

27 Kwa imani Mose aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme, alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho.

28 Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.

Imani Ya Mashujaa Wengine Wa Israeli

29 Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamukama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji.

30 Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba.

31 Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi.

32 Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii,

33 ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, walipokea ahadi za Mungu, walifunga vinywa vya simba,

34 walizima makali ya miali ya moto, waliepuka kuuawa kwa upanga, udhaifu wao ukageuka kuwa nguvu, walikuwa hodari vitani wakayashinda majeshi ya wageni na kuyafukuza.

35 Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi.

36 Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani.

37 Walipigwa kwa mawe, walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno, waliuawa kwa upanga, walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, waliteswa na kutendwa mabaya,

38 watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.

39 Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa.

40 Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/11-933f13d092f3ced43e2c0ccf2de158f4.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × four =