Wafilipi 2

Kuiga Unyenyekevu Wa Kristo

1 Kama kukiwa na jambo lo lote la kutia moyo, kukiwako faraja yo yote katika upendo, kukiwa na ushirika wo wote katika Roho, kukiwa na wema wo wote na huruma,

2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia kama hiyo, mkiwa na upendo huo huo, wenye roho moja na kusudi moja.

3 Msitende jambo lo lote kwa nia ya kujitukuza, bali kwa unyenyekevu, kila mtu akimhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake.

4 Kila mmoja wenu asiangalie mambo yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

5 Iweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

hakuona kule kuwa sawa na Mungu

ni kitu cha kushikilia,

7 bali alijifanya si kitu,

akajifanya sawa hasa na mtumwa,

akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

naam, mauti ya msalaba!

9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana

na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

la vitu vya mbinguni, vya duniani

na vya chini ya nchi,

11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

YESU KRISTO NI BWANA,

kwa utukufu wa Mungu Baba.

Ng’aeni Kama Mianga Katika Ulimwengu

12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka,

13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

14 Fanyeni mambo yote bila kunung’unika wala kushindana,

15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnang’aa kama mianga ulimwenguni.

16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.

17 Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote.

18 Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.

Paulo Amsifu Timotheo

19 Natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu.

20 Sina mtu mwingine kama yeye ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi.

21 Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Yesu Kristo.

22 Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana amefanya kazi ya Injili pamoja nami kama vile mwana kwa baba yake.

23 Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa.

24 Nami mwenyewe ninatumaini katika Bwana kwamba nitakuja kwenu hivi karibuni.

Paulo Amsifu Epafrodito

25 Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtenda kazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu.

26 Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa.

27 Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni.

28 Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue.

29 Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa,

30 kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake ili aweze kunipa msaada ambao ninyi hamkuweza kunipa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PHP/2-c4c4f604b469dca9baebdfea358fe437.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 × 3 =