Wagalatia 5

Uhuru Ndani Ya Kristo

1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia cho chote.

3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote.

4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu.

5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki.

6 Kwa maana ndani ya Kristo, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.

7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri, ni nani aliyewazuia msiitii kweli?

8 Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita.

9 “Chachu kidogo huchachua donge zima.”

10 Nina hakika katika Bwana kwa habari yenu kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu awaye yote anayewachanganya anastahili adhabu.

11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini basi bado niteswe na Wayahudi? Ukweli kwamba bado wananitesa, ni ushahidi kwamba bado ninahubiri wokovu kupitia msalaba wa Kristo peke yake.

12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!

13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo.

14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

Maisha Ya Kiroho

16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.

17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, nayo Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.

18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi,

20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake.

25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho.

26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GAL/5-0a09bd629b94c9a5d7636f4632568b9f.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eighteen − five =