Yohana 14

Yesu Awatia Moyo Wanafunzi Wake

1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia.

2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Nakwenda kuwaandalia makao.

3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo.

4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”

Yesu Ndiye Njia Ya Kwenda Kwa Baba

5 Tomasi akamwam bia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?”

6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.

7 Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”

8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.”

9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu ye yote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba?’

10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi.

11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo.

12 Amin, amin nawaambia, ye yote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba.

13 Nanyi mkiomba lo lote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana.

14 Kama mkiniomba lo lote kwa Jina langu nitalifanya.

Yesu Aahidi Roho Mtakatifu

15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.

16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele.

17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.

18 Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu.

19 Bado kitambo kidogo ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona, kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.

20 Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani yangu na mimi niko ndani yenu.

21 Ye yote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”

22 Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”

23 Yesu akamjibu, “Mtu ye yote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake.

24 Mtu ye yote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.

25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati nikiwa bado niko pamoja nanyi.

26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa nakwenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuliko mimi.

29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini.

30 Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu,

31 lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile vile kama Baba alivyoniamuru.

“Haya inukeni; twendeni zetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JHN/14-0e7ea4ae285c8489f93131c582f64b0e.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

5 × two =