1 Mambo ya Nyakati 19

Vita Dhidi Ya Waamoni

1 Baada ya muda, Nahashi mfalme wa Waamoni akafa, mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

2 Daudi akawaza, “Nitamtendea mema Hanuni mwana wa Nahashi, kwa sababu baba yake alinitendea mema.”

Hivyo Daudi akatuma wajumbe ili kumfariji Hanuni kwa ajili ya kifo cha baba yake. Watu wa Daudi walipofika kwa Hanuni katika nchi ya Waamoni ili kumfariji,

3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni, “Hivi unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kuwatuma wajumbe kukufariji? Je, hawa watu hawakuja kuipeleleza na kuidadisi nchi ili waishinde?”

4 Kwa hiyo Hanuni akawakamata wale watu wa Daudi, akawanyoa ndevu akakata nguo zao katikati kwenye matako, akawaondoa waende zao.

5 Mtu mmoja alipofika na kumpasha Daudi habari za watu hawa, akawatuma wajumbe wengine kuwalaki, kwa sababu waliaibishwa sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko mpaka ndevu zenu ziote, ndipo mrudi.”

6 Waamoni walipogundua kwamba wamekuwa harufu mbaya puani mwa Daudi, Hanuni na Waamoni wakatuma talanta 1,000za fedha ili kukodisha magari ya vita pamoja na waendeshaji wa hayo magari ya kukokotwa na farasi, kutoka Aramu-Naharaimu, Aramu-Maaka na Soba.

7 Wakakodisha magari ya vita 32,000 yakiwa na waendeshaji wake, pamoja na mfalme wa Maaka na vikosi vyake, wakaja na kupiga kambi karibu na Medeba. Waamoni nao wakakusanyika toka miji yao, wakatoka ili kupigana vita.

8 Daudi aliposikia juu ya haya, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji.

9 Waamoni wakatoka wakajipanga tayari kwa vita katika ingilio la mji wao, wakati ambapo wale wafalme wengine waliokuja nao walijipanga kwa vita uwanjani.

10 Yoabu akaona kwamba jeshi limejipanga mbele yake na nyuma yake, kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi bora katika Israeli na kuvipanga dhidi ya Waaramu.

11 Akawaweka wale wanajeshi wengine waliobaki chini ya amri ya Abishai ndugu yake, nao wakapangwa ili wakabiliane na Waamoni.

12 Yoabu akasema, “Kama Waamoni watanizidi nguvu, basi itakupasa wewe unisaidie, lakini kama Waamoni watakuzidi nguvu, basi mimi nitakusaidia.

13 Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu.Bwanaatafanya lile lililo jema machoni pake.”

14 Kisha Yoabu na vikosi vilivyokuwa pamoja naye wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia.

15 Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao pia wakakimbia mbele ya nduguye Abishai na kuingia ndani ya mji. Hivyo Yoabu, akarudi Yerusalemu.

16 Baada ya Waaramu kuona kwamba wamefukuzwa na Israeli, wakapeleka wajumbe na kuwataka Waaramu wengine kutoka ng’ambo ya Mto Eufrati, wakiongozwa na Shofaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri.

17 Daudi alipoelezwa haya, akawakusanya Israeli wote na kuvuka Yordani. Akasonga mbele dhidi yao na akajipanga kuwakabili. Daudi akapanga vita ili kupigana na Waaramu, nao wakapigana dhidi yake.

18 Lakini walikimbia mbele ya Israeli, Daudi akawaua waendesha magari 7,000 na askari wao wa miguu 40,000. Pia akamwua Shofaki, jemadari wa jeshi lao.

19 Raia wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya mapatano ya amani na Daudi, wakawa watumishi wake.

Hivyo Waaramu hawakukubali kuwasaidia Waamoni tena.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CH/19-c41b9e3074e3918643b971793a543252.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

seventeen + nine =