1 Petro 1

Salamu

1 Petro, mtume wa Yesu Kristo:

Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia.

2 Ninawaandikia ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utii na kunyunyizwa damu ya Yesu Kristo:

Neema iwe nanyi na amani iongezwe kwenu.

Tumaini Lenye Uzima

3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu,

4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,

5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho.

6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi.

7 Haya yamewajia ili kwamba uhalisi wa imani yenu (yenye thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto) ionekane kuwa katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atakapodhihirishwa.

8 Ambaye, ingawa hamjamwona, mnampenda, tena ingawa sasa hamumwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka.

9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

10 Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa,

11 wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata.

12 Mitume walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali walihudumu kwa ajili yenu katika mambo hayo ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo ambayo hata malaika wanatamani kuyafahamu.

Mwito Wa Kuishi Maisha Matakatifu

13 Kwa hiyo, vifungeni viuno vya nia zenu, mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa, Yesu Kristo atakapodhihirishwa.

14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya za kwanza za wakati wa ujinga.

15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote,

16 kwa maana imeandikwa: “Mtakuwa watakatifu, kwa kuwa Mimi ni mtakatifu.”

17 Nanyi kama mnamwita Baba yeye ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni.

18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo, yaani, kwa fedha na dhahabu,

19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, kama ile ya Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa.

20 Yeye aliwekewa hayo kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu,

21 ambaye kwa yeye mmemwamini Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.

22 Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli kwa njia ya Roho kwa kuwapenda ndugu zenu kwa upendo wa kweli, pendaneni kwa dhati kutoka moyoni.

23 Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu hata milele.

24 Maana,

“Watu wote ni kama majani,

na utukufu wao ni kama ua la shambani;

majani hunyauka na ua lake hupukutika,

25 lakini neno la Mungu ladumu milele.”

Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1PE/1-bb41903f01d07fc3c47798d12aa10f20.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 + six =