2 Petro 3

Ahadi Ya Kuja Kwa Bwana

1 Wapenzi, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha kwamba,

2 nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.

3 Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya,

4 wakisema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipokufa, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.”

5 Wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa hayo maji,

6 ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa na kuangamia.

7 Lakini kwa neno lilo hilo mbingu za sasa na dunia, zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.

8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili, kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu na miaka elfu ni kama siku moja.

9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake kama watu wengine wanavyodhani kukawia. Yeye anawavumilia, maana hataki mtu ye yote aangamie, bali kila mmoja afikilie toba.

10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu na vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.

11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, ninyi je, imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu,

12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu, ambayo siku hiyo mbingu zitachomwa moto na kutoweka na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto.

13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia kwa furaha mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.

14 Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia kwa furaha mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari.

15 Nanyi hesabuni uvumilivu wa Bwana kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu.

16 Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine.

17 Basi, ninyi wapenzi, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwenye uthabiti wenu.

18 Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2PE/3-53020c30f3ed70ee9ca17ac1560b72c3.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × 1 =