1 Wafalme 10

Malkia Wa Sheba Amtembelea Solomoni

1 Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina laBwana, malkia alikuja kumjaribu kwa maswali magumu.

2 Alipofika Yerusalemu pamoja na msafara mkubwa sana: pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani; alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake.

3 Solomoni akamjibu maswali yake yote, hakukuwa na jambo lo lote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea.

4 Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga,

5 chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu laBwana, alipatwa na mshangao.

6 Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli.

7 Lakini sikuamini mambo haya mpaka nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake, katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia.

8 Watu wako wanafurahi namna gani! Maafisa wako wanafurahi namna gani, wale ambao husimama mbele yako daima na kusikia hekima yako!

9 AhimidiweBwanaMungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka juu ya kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wakeBwanawa milele kwa ajili ya Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.”

10 Naye akampa mfalme talanta 120za dhahabu, kiasi kikubwa cha vikolezi na mawe ya thamani. Haikuwahi kamwe kutokea tena vikolezi vingi hivyo kuletwa kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni.

11 (Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena kutoka huko zilileta shehena kubwa ya miti ya msandali na mawe ya thamani.

12 Mfalme akatumia miti ya msandali kuwa nguzo kwa ajili ya Hekalu laBwanana kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha miti ya msandali hakijawahi kuingizwa nchini tangu siku ile.)

13 Mfalme Solomoni akampa malkia wa Sheba kila kitu alichohitaji na kukiomba, zaidi ya vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka akarudi pamoja na wafuasi wake kwenye nchi yake mwenyewe.

Fahari Ya Solomoni

14 Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666,

15 pasipo kuweka mapato kutoka wafanya biashara na wachuuzi, na kutoka kwa wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi.

16 Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600.

17 Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatuza dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.

18 Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi.

19 Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na egemeo la nyuma lilikuwa la mviringo kwa juu. Juu pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuwekea mikono, sanamu ya simba akisimama kila upande wake mahali pa kuwekea mikono.

20 Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, wawili kwenye kila ngazi, yaani, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wo wote.

21 Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Solomoni.

22 Mfalme alikuwa na meli nyingi za biasharabaharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wadogo na wakubwa.

23 Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia.

24 Dunia yote ikatafuta kukutana na Solomoni kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameweka katika moyo wake.

25 Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja alileta zawadi: vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu.

26 Solomoni akalimbikiza magari makubwa mazuri na farasi; alikuwa na magari 1,400 na farasi 12,000 ambayo aliyaweka katika miji ya magari pia pamoja naye huko Yerusalemu.

27 Mfalme akafanya fedha kuwa ya kawaida huko Yerusalemu kama mawe, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu chini ya vilima.

28 Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue; wafanyabiashara wa kifalme waliwanunua kutoka Kue.

29 Waliingiza magari kutoka Misri kwa bei ya shekeli za fedha 600na farasi kwa shekeli za fedha 150. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na Waaramu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/10-6409c8c690e73e8debb9d217df7b0f62.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

11 − four =