1 Wafalme 9

Bwana Anamtokea Solomoni

1 Solomoni alipomaliza kujenga Hekalu laBwanapamoja na jumba la kifalme, alipokwisha kufanya yote aliyotaka kufanya,

2 Bwanaakamtokea mara ya pili, kama alivyokuwa amemtokea huko Gibeoni.

3 Bwanaakamwambia:

“Nimesikia dua na maombi uliyofanya mbele zangu, nimeliweka wakfu Hekalu hili ambalo umelijenga, kwa kuweka Jina langu humo milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwa humo siku zote.

4 “Kukuhusu wewe, kama ukienenda kwa unyofu wa moyo na uadilifu, kama baba yako Daudi alivyofanya na kutenda yote ninayoyaagiza kwa kutunza maagizo yangu na sheria,

5 nitaimarisha kiti chako cha ufalme juu ya Israeli milele kama nilivyomwahidi Daudi baba yako nikisema, ‘Hutakosa kamwe kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’

6 “Lakini kama ninyi au wana wenu wakigeukia mbali nami na kuziacha amri na maagizo yangu niliyowapa na kwenda kuwatumikia miungu mingine na kuiabudu,

7 basi nitakatilia mbali Israeli kutoka katika nchi niliyowapa na kulikataa Hekalu hili nililoliweka wakfu kwa Jina langu. Ndipo Israeli itakuwa kitu cha kudharauliwa na watu na kuwa kitu cha mzaha miongoni mwa watu wote.

8 Ingawa Hekalu hili linavutia sasa, wote watakaopita karibu yake watashangaa na kudhihaki wakisema, ‘Kwa niniBwanaamefanya kitu cha namna hii katika nchi hii na kwenye Hekalu hili?’

9 Watu watajibu, ‘Kwa sababu wamemwachaBwanaMungu wao, aliyewatoa baba zao Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakiiabudu na kuitumikia, ndiyo sababuBwanaameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”

Shughuli Nyingine Za Solomoni

10 Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Solomoni alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu laBwanana jumba la kifalme,

11 Mfalme Solomoni akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi yote, misunobari na dhahabu yote aliyohitaji.

12 Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Solomoni alikuwa amempa, hakupendezwa nayo.

13 Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?”

# Naye akaiita nchi ya Kabul, jina lililoko hadi leo.

14 Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta 120za dhahabu.

15 Haya ni maelezo kuhusu Mfalme Solomoni, jinsi alivyowafanyiza watu kazi za kulazimishwa ili kulijenga Hekalu laBwana, jumba la kifalme kwa ajili yake mwenyewe, Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri.

16 (Farao mfalme wa Misri alikuwa ameshambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Solomoni, kama zawadi ya arusi.

17 Solomoni akaujenga tena upya Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini,

18 akajenga pia Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake,

19 vile vile miji ya ghala na miji kwa ajili ya magari yake na farasi wake: cho chote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni na katika nchi yote iliyokuwa chini ya mamlaka yake.

20 Watu wote waliobaki kutoka kwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (mataifa haya hayakuwa Waisraeli),

21 yaani, uzao wao uliobaki katika nchi, ambao Waisraeli wasingeweza kuwaangamiza, hawa Solomoni akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo.

22 Lakini Solomoni hakumfanya ye yote wa Waisraeli kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa wapiganaji wake, maafisa wake wa serikali, maafisa wake, wakuu wake, majemadari wa jeshi wa magari yake ya vita na wapanda farasi.

23 Pia walikuwa maafisa wakuu wasimamizi wa miradi ya Solomoni: maafisa 550 waliowasimamia watu waliofanya kazi.

24 Baada ya binti Farao kuja kutoka Mji wa Daudi na kuingia katika jumba la kifalme Solomoni alilokuwa amemjengea, akajenga Milo.

25 Solomoni akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani mara tatu kwa mwaka, juu ya madhabahu aliyokuwa amejenga kwa ajili yaBwana, akifukiza uvumba mbele zaBwanapamoja na dhabihu hizo, hivyo kutimiza kanuni za Hekalu.

26 Mfalme Solomoni akatengeneza pia meli huko Ezion-Geberi, ambayo iko karibu na Elathi katika Edomu, kwenye ukingo wa Bahari ya Shamu.

27 Naye Hiramu akatuma watu wake, mabaharia walioijua bahari, kuhudumu katika hizo meli pamoja na watu wa Solomoni.

28 Wakasafiri kwenda Ofiri na kurudi na talanta 420za dhahabu, ambazo walimletea Mfalme Solomoni.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1KI/9-b98f8502b4f443b4ac84ba6596c45db7.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

19 − 6 =