1 Wakorintho 10

Onyo Kutoka Historia Ya Waisraeli

1 Zaidi ya hayo ndugu zangu, sitaki mkose kufahamu ukweli huu kwamba baba zetu walikuwa wote chini ya wingu na kwamba wote walipita katikati ya bahari.

2 Wote wakabatizwa kuwa wa Mose ndani ya lile wingu na ndani ya ile bahari.

3 Wote walikula chakula kile cha roho,

4 na wote wakanywa kile kinywaji cha roho, kwa maana walikunywa kutoka katika ule mwamba wa roho uliofuatana nao, nao ule mwamba ulikuwa Kristo.

5 Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, kwa hiyo miili yao ilitapakaa jangwani.

6 Basi mambo haya yalitokea kama mfano ili kutuonya tusiweke mioyo yetu katika mambo maovu kama wao walivyofanya.

7 Msiwe waabudu sanamu, kama baadhi yao walivyokuwa, kama ilivyoandikwa, “Watu walikaa chini wakala na kunywa, kisha wakainuka kucheza na kufanya karamu za kipagani.”

8 Wala tusifanye uzinzi kama baadhi yao walivyofanya, wakafa watu 23,000 kwa siku moja.

9 Wala tusimjaribu Bwana, kama baadhi yao walivyofanya, wakafa kwa kuumwa na nyoka.

10 Msinung’unike kama baadhi yao walivyofanya, wakaangamizwa na mharabu.

11 Mambo haya yote yaliwapata wao ili yawe mifano kwa wengine, nayo yaliandikwa ili yatuonye sisi ambao mwisho wa nyakati umetufikia.

12 Hivyo, yeye ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke.

13 Hakuna jaribu lo lote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu ambaye hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

Karamu Za Sanamu Na Meza Ya Bwana

14 Kwa hiyo wapenzi wangu, zikimbieni ibada za sanamu.

15 Nasema nanyi kama na watu wenye ufahamu, amueni wenyewe kuhusu haya niyasemayo.

16 Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Kristo? Mkate tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?

17 (Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja).

18 Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni?

19 Je, nina maana kwamba kafara iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yo yote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yo yote?

20 La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani.

21 Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.

22 Je, tunataka kuamsha wivu wa Bwana? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?

Fanyeni Yote Kwa Utukufu Wa Mungu

23 “Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga.

24 Mtu ye yote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.

25 Kuleni cho chote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lo lote kwa ajili ya dhamiri.

26 Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.”

27 Kama ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri.

28 Lakini kama mtu ye yote akikuambia, “Hiki kimetolewa kafara kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri.

29 Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine?

30 Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?

31 Basi, lo lote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.

32 Msiwe kikwazo kwa mtu ye yote, kwa Wayahudi au kwa Wayunani, au kwa Kanisa la Mungu,

33 kama mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali mema kwa ajili ya faida ya wengi, ili waweze kuokolewa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/10-bb7318c28718f7ef5a84c831700bca42.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 × 1 =