1 Wakorintho 9

Haki Za Mtume

1 Je, mimi si huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu, Bwana wetu? Je, ninyi si matunda ya kazi yangu katika Bwana?

2 Hata kama mimi si mtume kwa wengine, hakika mimi ni mtume kwenu, kwa maana ninyi ni chapa ya utume wangu katika Bwana.

3 Huu ndio utetezi wangu kwa hao wanaokaa kunihukumu.

4 Je, hatuna haki ya kula na kunywa?

5 Je, hatuna haki ya kusafiri na mke anayeamini, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu zake Bwana na Kefa?

6 Au ni mimi na Barnaba tu ambao tunalazimika kufanya kazi ili tuweze kupata mahitaji yetu?

7 Ni askari yupi aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Ni mkulima gani apandaye shamba la mizabibu na asile matunda yake? Ni nani achungaye kundi na asipate maziwa yake hata kidogo?

8 Je, nasema mambo haya katika mtazamo wa kibinadamu tu? Je, sheria haisemi yayo hayo?

9 Kwa maana imeandikwa katika Sheria ya Mose: “Usimfunge ng’ombe kinywa apurapo nafaka.” Je, Mungu hapa anahusika na ng’ombe?

10 Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mwingine akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno.

11 Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, Je, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu?

12 Kama wengine wana haki ya kupata msaada kutoka kwenu, sisi je, isingepasa tuwe na haki hiyo hata zaidi?

Lakini sisi hatukutumia haki hii. Kinyume chake, tunavumilia kila kitu ili tusije tukazuia injili ya Kristo.

13 Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi Hekaluni hupata chakula chao kutoka Hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni?

14 Vivyo hivyo, Bwana ameagiza kwamba wale wanaohubiri injili wapate mahitaji yao kutokana na injili.

15 Lakini sijatumia hata mojawapo ya haki hizi. Nami siandiki haya nikitumaini kwamba mtanifanyia mambo hayo. Heri nife kuliko mtu ye yote kuninyima huku kujisifu kwangu.

16 Lakini ninapohubiri injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili!

17 Nikihubiri kwa hiari ninayo thawabu, lakini kama si kwa hiari, ni kwamba nalazimika kufanya hivyo, basi ninachofanya ni kutekeleza tu uwakili niliowekewa.

18 Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ni kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, nisije nikatumia vibaya ule uwezo wangu nilio nao katika Injili.

19 Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu ye yote, nimejifanya kuwa mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi zaidi.

20 Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama aliye chini ya sheria (ingawa mimi siko chini ya sheria), ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria.

21 Kwa watu wasio na Sheria nilikuwa kama asiye na Sheria (ingawa siko huru mbali na Sheria ya Mungu, bali niko chini ya Sheria ya Kristo), ili niweze kuwapata wale wasio na Sheria.

22 Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yo yote niweze kuwaokoa baadhi yao.

23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.

24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano kwa jinsi ambavyo mtapata tuzo.

25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele.

26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa,

27 la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/9-dbd225cdb0b3c985857d920bedd822de.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

fourteen − two =