1 Wakorintho 4

Mawakili Wa Siri Za Mungu

1 Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu.

2 Zaidi ya hayo, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu.

3 Lakini kwangu mimi ni jambo dogo sana kwamba nihukumiwe na ninyi au na mahakama yo yote ya kibinadamu. Hata mimi mwenyewe sijihukumu.

4 Dhamiri yangu ni safi, lakini hilo halinifanyi nisiwe na hatia. Bwana ndiye anihukumuye.

5 Kwa hiyo msihukumu jambo lo lote kabla ya wakati wake, ngojeni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

6 Basi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kuwa mfano wa mimi binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine.

7 Kwa maana ni nani aliyekufanya wewe kuwa tofauti na mwingine? Ni nini ulicho nacho ambacho hukupokea? Nawe kama ulipokea, kwa nini unajivuna kama vile hukupokea?

8 Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi!

9 Kwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa, kwa sababu tumefanywa kuwa maonyesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia.

10 Kwa ajili ya Kristo sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima ndani ya Kristo. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa.

11 Mpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao.

12 Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili,

13 tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Mpaka sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu hadi leo.

14 Siwaandikii mambo haya ili kuwaaibisha, bali ili kuwaonya, kama wanangu wapendwa.

15 Hata kama mnao walimu 10,000 katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Kristo Yesu kwa kuwaletea Injili.

16 Basi nawasihi igeni mfano wangu.

17 Kwa sababu hii ninamtuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana. Yeye atawakumbusha kuhusu maisha yangu katika Kristo ambayo yanakubaliana na mafundisho yangu ninayofundisha kila mahali kwenye kila kanisa.

18 Baadhi yenu mmekuwa na majivuno mkidhani kuwa sitafika kwenu.

19 Lakini kama Bwana akipenda, nitafika kwenu mapema, nami nitapenda kujua, si tu kile wanachosema hawa watu wenye kiburi, bali pia kujua nguvu yao.

20 Kwa kuwa Ufalme wa Mungu si maneno matupu tu bali ni nguvu.

21 Ninyi amueni. Je, nije kwenu na fimbo, au nije kwa upendo na kwa roho ya upole?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/4-62bb6e9537f1f502f485c8872c8c1a9b.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

fifteen + seventeen =