1 Wakorintho 3

Kuhusu Mgawanyiko Katika Kanisa

1 Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Kristo.

2 Naliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula kigumu. Naam, hata sasa hamkiwezi.

3 Kwa maana ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini, nanyi mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?

4 Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida?

5 Kwani, Apolo ni nani? Naye Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kwa kupitia wao mliamini.

6 Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliyekuza.

7 Hivyo mwenye kupanda mbegu na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ndiye akuzaye.

8 Apandaye mbegu ni sawa na yule atiaye maji. Kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake.

9 Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu, ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.

10 Kwa neema Mungu aliyonipa, niliweka msingi kama mjenzi stadi na mtu mwingine anajenga juu ya huo msingi. Lakini kila mmoja inampasa awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake.

11 Kwa maana hakuna mtu ye yote awezaye kuweka msingi mwingine wo wote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Yesu Kristo.

12 Kama mtu ye yote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, mawe ya thamani, miti, majani au nyasi,

13 kazi yake itaonekana kuwa ikoje, kwa kuwa siku ile itaidhihirisha kazi yake. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu.

14 Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu.

15 Kama kazi ya mtu itateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini kama mtu aliyenusurika kwenye moto.

16 Je, hamjui ya kwamba ninyi ni Hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu ye yote akiliharibu Hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza mtu huyo, Kwa maana Hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

18 Msijidanganye. Kama mtu ye yote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima.

19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,”

20 Tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.”

21 Hivyo basi, mtu asijivune kuhusu wanadamu! Kwa kuwa vitu vyote ni vyenu,

22 ikiwa ni Paulo au Apolo au Kefaau dunia au uzima au mauti, au wakati uliopo au wakati ujao, haya yote ni yenu

23 na ninyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/3-460093c974171613041a242f57f32e09.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 × two =