1 Wakorintho 6

Kushtakiana Miongoni Mwa Waamini

1 Kama mtu ye yote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu?

2 Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo?

3 Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya?

4 Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya ninyi mwachagua watu ambao hata hawaheshimiwi katika kanisa kuwa waamuzi?

5 Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya ndugu mmoja na mwenzake?

6 Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!

7 Ukweli ni kwamba huko kuwa na mashtaka dhidi ya mwingine miongoni mwenu tayari ni kushindwa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyang’anywa?

8 Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.

9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati hawaurithi Ufalme wa Mungu, wala waombao sanamu, wala wahanithi, wala walawiti,

10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walafi, wala wanaodhihaki, wala wanyang’anyi.

11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

Dhambi Za Zinaa

12 “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu cho chote.

13 “Chakula ni kwa ajili ya tumbo na tumbo ni kwa ajili ya chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili wa mwanadamu haukuumbwa kwa ajili ya zinaa bali kwa ajili ya Bwana na Bwana kwa ajili ya mwili.

14 Naye Mungu aliyemfufua Bwana kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza wake.

15 Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Kristo? Je, nichukue viungo vya mwili wa Kristo na kuviunganisha na mwili wa kahaba? La hasha!

16 Hamjui kwamba aliyeungwa na kahaba anakuwa mwili mmoja naye? Kwa kuwa imenenwa, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.”

17 Lakini mtu aliyeungwa na Bwana anakuwa roho moja naye.

18 Ikimbieni zinaa. Dhambi nyingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe.

19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni Hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe,

20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu na katika roho zenu ambazo ni mali ya Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/6-f2eb8bcc6623ec8de949f95d94963db8.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eighteen − twelve =