1 Wakorintho 7

Kuhusu Ndoa

1 Basi kuhusu mambo yale mliyoniandikia: Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke.

2 Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe.

3 Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe.

4 Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe.

5 Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi.

6 Nasema haya kama ushauri na si amri.

7 Laiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.

8 Kwa wale wasiooa na kwa wajane, ingekuwa vizuri wabaki kama mimi nilivyo.

9 Lakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.

10 Kwa wale waliooana nawapa amri (si mimi ila ni Bwana): Mke asimwache mumewe.

11 Lakini kama akimwacha, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.

12 Lakini kwa wengine nasema (si Bwana ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache.

13 Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache.

14 Kwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe. Kama isingalikuwa hivyo watoto wenu wangalikuwa si safi, lakini ilivyo sasa wao ni watakatifu.

15 Lakini kama yule asiyeamini akijitenga, basi afanye hivyo. Katika hali kama hiyo mwanamke au mwanaume aaminiye hafungwi, kwa sababu Mungu ametuita tuishi kwa amani.

16 Wewe mke, unajuaje kama utamwokoa mumeo? Au wewe mume unajuaje kama utamwokoa mkeo?

Kuishi Kama Alivyoagiza Bwana

17 Lakini kila mtu na aishi maisha aliyopangiwa na Bwana, yale Mungu aliyokuitia. Hii ni sheria yangu kwa makanisa yote.

18 Je, mtu alikuwa ametahiriwa alipoitwa? Asijifanye asiyetahiriwa. Je, mtu alikuwa hajatahiriwa alipoitwa? Asitahiriwe.

19 Kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu. Lakini kuzitii amri za Mungu ndilo jambo muhimu.

20 Basi kila mmoja wenu na abaki katika hali aliyoitwa nayo.

21 Je, wewe ulipoitwa ulikuwa mtumwa? Jambo hilo lisikusumbue. Hata kama unaweza kupata uhuru, tumia nafasi uliyo nayo sasa kuliko wakati mwingine wo wote.

22 Kwa maana ye yote aliyeitwa katika Bwana kama mtumwa yeye ni mtu huru kwa Bwana, kama vile ye yote aliyekuwa huru alipoitwa yeye ni mtumwa wa Kristo.

23 Mlinunuliwa kwa gharama, ili msiwe watumwa wa wanadamu.

24 Ndugu zangu, kama kila mtu alivyoitwa, akae katika wito wake alioitiwa na Mungu.

Wajane Na Wasioolewa

25 Basi, kuhusu wale walio bikira, mimi sina amri kutoka kwa Bwana, lakini mimi natoa shauri kama mtu ambaye ni mwaminifu kwa rehema za Bwana.

26 Kwa sababu ya shida iliyoko, naona ni vyema mkibaki kama mlivyo.

27 Je, umeolewa? Basi usitake talaka. Je, hujaoa? Usitafute mke.

28 Lakini kama ukioa, hujatenda dhambi; na kama bikira akiolewa, hajatenda dhambi. Lakini wale wanaooa watakabiliana na matatizo mengi katika maisha haya, nami nataka kuwazuilia hayo.

29 Lakini ndugu zangu, nina maana kwamba muda uliobaki ni mfupi. Tangu sasa wale waliooa waishi kama wasio na wake;

30 nao wanaoomboleza, kama ambao hawaombolezi; wenye furaha kama wasiokuwa nayo; wale wanaonunua, kama vile vitu walivyonunua si mali yao;

31 nao wale wanaoshughulika na vitu vya dunia hii, kama ambao hawahusiki navyo. Kwa maana dunia hii kama tunavyoiona sasa inapita.

32 Ningetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana, yaani, jinsi ya kumpendeza Bwana.

33 Lakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, yaani, jinsi ya kumfurahisha mkewe,

34 pia kuna tofauti kati ya mwanamke aliyeolewa na msichana bikira. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana ili awe mtakatifu kimwili na kiroho, lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe.

35 Ninasema haya kwa faida yenu, sio ili kuwawekea kizuizi cho chote, bali mpate kuishi kwa jinsi ilivyo vyema bila kuvutwa pengine katika kujitoa kwenu kwa Bwana.

36 Kama mtu ye yote anadhani kwamba hamtendei ilivyo sawa mwanamwali ambaye amemposa, naye akiwa umri wake unazidi kuendelea na mtu huyo anajisikia kwamba inampasa kuoa, afanye kama atakavyo. Yeye hatendi dhambi. Yawapasa waoane.

37 Lakini kama mwanaume ambaye ameshaamua moyoni mwake kutokuoa bila kulazimishwa na mtu ye yote, kama anaweza kujitawala kabisa; basi anafanya vyema kutokumwoa huyo mwanamwali.

38 Hivyo basi, yeye mwanaume amwoaye huyo mwanamwali afanya vyema, lakini yeye asiyemwoa afanya vyema zaidi.

39 Mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria maadamu mumewe yu hai. Lakini kama mumewe akifa, basi mwanamke huyo yuko huru kuolewa na mume mwingine ampendaye, lakini lazima tu awe katika Bwana.

40 Lakini kwa uamuzi wangu, naona kuwa angekuwa na furaha zaidi akibaki alivyo. Nami nadhani pia nina Roho wa Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/7-5ac4c955c1a23ab3bedca62b743e7739.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

sixteen − 3 =