1 Wathesalonike 4

Maisha Yanayompendeza Mungu

1 Hatimaye, ndugu, tuliwaomba na kuwasihi katika Bwana Yesu kwamba, kama mlivyojifunza kutoka kwetu jinsi iwapasavyo kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi, imewapasa mzidi sana kufanya hivyo.

2 Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

3 Kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu ninyi mwe watakatifu, ili kwamba mjiepushe na uasherati,

4 ili kwamba kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima,

5 si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu.

6 Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Bwana ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali.

7 Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu.

8 Kwa hiyo, mtu ye yote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

9 Sasa kuhusu upendano wa ndugu hamna haja mtu ye yote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.

10 Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.

11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza,

12 ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu ye yote.

Kuja Kwake Bwana

13 Lakini ndugu, hatutaki msijue kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini.

14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, hata hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mauti katika yeye.

15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe tunawaambia kwamba, sisi ambao bado tuko hai, tutakaobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wale waliolala mauti.

16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka toka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu pamoja na sauti ya malaika mkuu na sauti ya tarumbeta ya Mungu, nao wale waliolala mauti wakiwa wanamwamini Kristo watafufuka kwanza.

17 Baada ya hilo sisi tulio hai bado, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TH/4-d9f2fc62eb99b12a94f50e9a4d4ced21.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

nine − three =