1 Wathesalonike 5

Iweni Tayari Kwa Siku Ya Bwana

1 Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia,

2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwivi ajapo usiku.

3 Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba wala hawatatoroka.

4 Bali ninyi, ndugu, hamko gizani hata kwamba siku ile iwakute ghafula kama mwivi.

5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku.

6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi.

7 Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku.

8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo.

9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili kwamba kama tuko macho au tukiwa tumelala tupate kuishi pamoja naye.

11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.

Maagizo Ya Mwisho, Salamu Na Kuwatakia Heri

12 Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya.

13 Mkawajali sana katika upendo kwa ajili ya kazi yao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.

14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni wale wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na iweni na uvumilivu na kila mtu.

15 Angalieni kuwa mtu asilipe ovu kwa ovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

16 Furahini siku zote;

17 ombeni pasipo kukoma;

18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

19 Msiuzime moto wa Roho Mtakatifu;

20 msiyadharau maneno ya unabii.

21 Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema.

22 Jiepusheni na uovu wa kila namna.

23 Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo.

24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.

25 Ndugu, tuombeeni.

26 Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu.

27 Nawaagizeni mbele za Bwana mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii.

28 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1TH/5-9e5b0ece028ec883a54dc818e52749aa.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three + 2 =