2 Mambo ya nyakati 16

Miaka Ya Mwisho Ya Mfalme Asa

1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa kutawala kwa Asa, Mfalme Baasha wa Israeli akaishambulia Yuda na kuujengea ngome mji wa Rama ili kumzuia ye yote asitoke wala kuingia katika nchi ya Mfalme Asa wa Yuda.

2 Ndipo Asa akachukua fedha na dhahabu kutoka katika hazina ya Hekalu laBwanana kutoka katika jumba lake mwenyewe la kifalme na kumpelekea Ben-Hadadi mfalme wa Aramu, ambaye alikuwa anatawala huko Dameski.

3 Akasema, “Pawepo na makubaliano kati yangu na wewe, kama yalivyokuwako kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, ninakupelekea fedha na dhahabu. Basi vunja makubaliano yako na Mfalme Baasha wa Israeli ili aweze kujiondoa huku kwangu.”

4 Ben-Hadadi akakubaliana na Mfalme Asa na kutuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Wakashinda Iyoni, Dani, Abel-Maimu na miji yote ya hazina ya Naftali.

5 Baasha aliposikia jambo hili, akasimamisha kujenga Rama na kuacha kazi yake.

6 Ndipo Mfalme Asa akawaleta watu wote wa Yuda, nao wakachukua mawe na miti ambayo Baasha alikuwa anavitumia huko Rama. Kwa vitu hivyo akajenga Geba na Mizpa.

7 Ikawa wakati huo mwonaji Hanani akamjia Mfalme Asa wa Yuda na kumwambia: “Kwa sababu ulimtegemea mfalme wa Aramu nawe hukumtegemeaBwanaMungu wako, jeshi la mfalme wa Aramu limeponyoka mkononi mwako.

8 Je, hukumbuki lililotendeka kwa Wakushi na Walibya, hawakuwa jeshi lenye nguvu na magari mengi ya vita na wapanda farasi? Hata hivyo, ulipomtegemeaBwanayeye aliwatia mkononi mwako.

9 Kwa kuwa macho yaBwanahukimbiakimbia duniani kote ili kujionyesha mwenye nguvu kwa ajili ya wale ambao mioyo yao inamtegemea kwa ukamilifu. Umefanya jambo la upumbavu na kuanzia sasa na kuendelea utakuwa na vita.”

10 Asa akamkasirikia mwonaji kwa sababu ya jambo hili. Alikuwa ameghadhibika sana hata akamweka gerezani. Wakati huo huo Asa akaanza kuwatesa na kuwaonea baadhi ya watu kwa ukatili.

11 Matukio ya utawala wa Asa, kuanzia mwanzo mpaka mwisho, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

12 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wake, Asa alipatwa na ugonjwa kwenye miguu yake. Ingawa ugonjwa wake ulimzidia sana, hata katika kuugua kwake hakutafuta msaada kutoka kwaBwanabali kwa matabibu tu.

13 Ndipo katika mwaka wa arobaini na moja wa kutawala kwake Asa, akafa na kulala na baba zake.

14 Nao wakamzika katika kaburi lile alilokuwa amelichonga kwa ajili yake mwenyewe katika Mji wa Daudi. Wakamzika kwa jeneza lililowekwa vikolezi na mchanganyiko wa manukato ya aina mbalimbali yaliyotengenezwa kwa utaalamu wa mtengeneza marashi, nao wakawasha moto mkubwa kwa heshima yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/16-b5e4d38dff0ca430fc83a88e91b8ff29.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

11 + eleven =