2 Mambo ya nyakati 34

Yosia Afanya Matengenezo

1 Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka thelathini na mmoja.

2 Akafanya yaliyo mema machoni paBwanana kuenenda katika njia za Daudi baba yake, pasipo kugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.

3 Katika mwaka wa nane wa utawala wake, alipokuwa angali bado mdogo, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi baba yake. Katika mwaka wake wa kumi na mbili alianza kusafisha mahali pa juu pa kuabudia miungu pa Yuda na Yerusalemu, akiondoa nguzo za Ashera, sanamu za kuchonga na vinyago vya kusubu.

4 Mbele ya macho yake, wakazibomoa madhabahu za Mabaali, wakazivunja madhabahu za kufukizia uvumba zilizokuwa zimesimama juu yake, wakazivunja nguzo za Ashera, sanamu na vinyago. Hivi alivivunja vipande vipande na kuvisambaza juu ya makaburi ya waliokuwa wamevitolea kafara.

5 Akachoma mifupa ya makuhani wao juu ya madhabahu zao na kwa njia hiyo akaitakasa Yuda na Yerusalemu.

6 Katika miji ya Manase, Efraimu na Simeoni, hadi Naftali na kwenye magofu yanayoizunguka,

7 akavunja madhabahu na nguzo za Ashera na kuzipondaponda hizo sanamu hadi zikawa unga na kukata vipande vipande madhabahu zote za kufukizia uvumba katika Israeli yote. Kisha akarudi Yerusalemu.

8 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yosia, ili kutakasa nchi na Hekalu, akawatuma Shafani, mwana wa Azalia na Maaseya mtawala wa mji, pamoja na Yoa mwana wa Yoahazi, mwandishi ili kukarabati Hekalu laBwanaMungu wake.

9 Wakamwendea Hilkia kuhani mkuu na kumpa fedha ambazo zilikuwa zimeletwa ndani ya Hekalu laBwanaambazo Walawi waliokuwa mabawabu walikuwa wamezikusanya kutoka kwa watu wa Manase, Efraimu na mabaki wote wa Israeli kutoka kwa watu wote wa Yuda na Benyamini na wakazi wa Yerusalemu.

10 Kisha wakazikabidhi hizo fedha kwa watu waliowekwa ili kusimamia kazi ya Hekalu laBwana. Hawa watu waliwalipa wafanyakazi waliokarabati na kutengeneza Hekalu lipate kurudi katika hali yake.

11 Wakawapa pia mafundi seremala na waashi fedha ili kununua mawe yaliyochongwa, mbao kwa ajili ya kufungia na boriti kwa ajili ya majengo ambayo wafalme wa Yuda walikuwa wameyaacha yakawa magofu.

12 Watu wakafanya kazi kwa uaminifu. Waliokuwa wamewekwa juu yao ili kuwaelekeza ni Yahathi na Obadia, Walawi wa uzao wa Merari, Zekaria na Meshulamu, waliotoka kwenye uzao wa Kohathi. Walawi wote waliokuwa na ufundi wa kupiga ala za uimbaji,

13 wakawa wasimamizi wa vibarua na kuwaongoza wale waliofanya kila aina ya kazi. Baadhi ya Walawi walikuwa, waandishi, maafisa na mabawabu.

Kitabu Cha Sheria Chapatikana

14 Wakati walipokuwa wakizitoa nje zile fedha zilizokuwa zimetolewa kwenye Hekalu laBwanakuhani Hilkia akakipata kile Kitabu cha Sheria yaBwanakilichokua kimetolewa kwa mkono wa Mose.

15 Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, “nimekiona Kitabu cha Sheria ndani ya Hekalu laBwana.” Akampatia Shafani kile Kitabu.

16 Ndipo Shafani akakipeleka kile Kitabu kwa mfalme na kumwambia, “Maafisa wako wanafanya kila kitu kama walivyokabidhiwa kufanya.

17 Wamelipa fedha zilizokuwa katika Hekalu laBwanana wamewakabidhi wasimamizi na wafanyakazi.”

18 Kisha Shafani mwandishi akamwarifu mfalme kuwa, “Kuhani Hilkia amenipatia Kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.

19 Mfalme aliposikia yale maneno ya Sheria, akayararua mavazi yake.

20 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, Shafani mwandishi na Asaya mtumishi wa mfalme,

21 “Nendeni mkamwulizeBwanakwa ajili yangu na kwa ajili ya mabaki walioko Israeli na Yuda kuhusu haya yaliyoandikwa katika kitabu hiki ambacho kimeonekana hekaluni. Hasira yaBwanani kubwa mno ambayo imemwagwa juu yetu kwa sababu baba zetu hawakulishika neno laBwanawala hawakutenda sawasawa na yale yote yaliyoandikwa katika Kitabu hiki.”

22 Hilkia pamoja na wale wote mfalme aliokuwa amewatuma pamoja naye wakaenda kuzungumza na nabii mke aitwaye Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tokhathi, mwana wa Hasra mtunzaji wa kabati la mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu, katika Mtaa wa Pili.

23 Akawaambia, “Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli asemalo, mwambieni mtu huyo aliyewatuma kwangu,

24 ‘Hili ndiloBwanaasemalo: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, laana zote zilizoandikwa ndani ya hicho kitabu ambazo zimesomwa mbele ya mfalme wa Yuda.

25 Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine ili waichochee hasira yangu kwa kazi yote ya mikono yao, hivyo hasira yangu itamwagwa juu ya mahali hapa, wala haitatulizwa.

26 Mwambieni mfalme wa Yuda, aliyewatuma kumwulizaBwana, Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu maneno uliyoyasikia:

27 Kwa sababu moyo wako ulikuwa mwepesi kusikia, nawe ukajinyenyekeza mbele za Mungu wakati uliposikia kile alichokisema dhidi ya mahali hapa na watu wake na kwa sababu ulijinyenyekeza mbele zangu ukararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asemaBwana.

28 Basi nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa na juu ya wote wanaoishi hapa.’ ”

Kwa hiyo wakampelekea mfalme jibu lake.

29 Ndipo mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.

30 Akapanda kwenda hekaluni mwaBwanapamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na Walawi, yaani watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi mkubwa kabisa. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu laBwana.

31 Mfalme akasimama karibu na nguzo yake na kufanya upya Agano mbele zaBwanaili kumfuataBwanana kuzishika amri zake, maagizo na sheria kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote na ili kuyatii maneno ya Agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

32 Ndipo akamtaka kila mmoja katika Yerusalemu na Benyamini kuweka ahadi zao wenyewe kwa hilo Agano, watu wa Yerusalemu wakafanya hivyo kwa kufuata Agano laBwana, Mungu wa baba zao.

33 Yosia akaondoa machukizo yote ya sanamu kutoka katika nchi yote iliyokuwa mali ya Waisraeli na akawataka wale wote waliokuweko katika Israeli wamtumikieBwanaMungu wao. Kwa muda wote alioishi, hawakushindwa kumfuataBwana, Mungu wa baba zao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/34-c0109b8dbe62dca2feb91f1ab080952b.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 + 8 =