2 Mambo ya nyakati 4

Vifaa Vya Hekalu

1 Mfalme Solomoni akatengeneza madhabahu ya shaba yenye urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini na kimo chake dhiraa kumi.

2 Akatengeneza Bahari ya kusubu, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo na kina chake kilikuwa dhiraa tano. Kamba ya urefu wa dhiraa thelathiniingeweza kuizunguka.

3 Chini ya huo ukingo, kulikuwa na mafahali kuizunguka, yaani mafahali kumi katika kila dhiraa moja. Hayo mafahali waliyasubu katika safu mbili yakiwa ya kitu kimoja na hiyo Bahari.

4 Bahari hiyo ilikaa juu ya mafahali kumi na mawili, mafahali matatu yalielekeza nyuso zao kaskazini, matatu magharibi, matatu kusini na matatu mashariki. Bahari hiyo ilikaa juu ya hao mafahali, nazo sehemu zao za nyuma zilielekea katikati.

5 Unene wake ulikuwa nyanda nne, ambao ulikuwa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi li lililochanua. Bahari hii iliweza kuchukua kiasi cha bathi 3,000.

6 Kisha akatengeneza masinia kumi kwa ajili ya kuoshea vifaa, naye akayaweka matano upande wa kusini na matano upande wa kaskazini. Ndani yake ndimo vilimooshewa vifaa vya kutumika katika sadaka za kuteketezwa, lakini ile Bahari ilikuwa ni kwa ajili ya makuhani kunawia.

7 Akatengeneza vinara vya taa kumi vya dhahabu kama ilivyoainishwa kwao na kuviweka hekaluni, vinara vitano upande wa kusini na vitano upande wa kaskazini.

8 Akatengeneza meza kumi na kuziweka hekaluni, tano upande wa kusini na tano upande wa kaskazini. Pia akatengeneza mabakuli 100 ya dhahabu ya kunyunyizia.

9 Akatengeneza ukumbi wa makuhani na ukumbi mwingine mkubwa na milango yake, naye akaifunika hiyo milango kwa shaba.

10 Akaweka ile Bahari upande wa kusini, kwenye pembe ya kusini mashariki ya nyumba.

11 Pia akatengeneza masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.

Kwa hiyo Huramu akamaliza kazi aliyokuwa amefanya kwa ajili ya Mfalme Solomoni katika Hekalu la Mungu:

12 zile nguzo mbili;

yale mataji mawili yaliyokuwa juu ya hizo nguzo,

zile nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli yaliyowekwa juu ya zile nguzo;

13 yale makomamanga 400 kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu yakipamba hizo nyavu mbili zilizowekwa juu ya zile nguzo);

14 vishikio pamoja na masinia yake;

15 hiyo Bahari na hao mafahali kumi na wawili chini yake;

16 pia hayo masufuria, masepetu, nyuma za nyama na vyombo vingine vyote vilivyohusiana.

Vitu vyote ambavyo Huramu-Abi alimtengenezea Mfalme Solomoni kwa ajili ya Hekalu laBwanavilikuwa vya shaba iliyosuguliwa.

17 Mfalme aliagiza wavisubu vitu hivi kwenye kalibu za udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani kati ya Sukothi na Seredatha.

18 Vitu hivi vyote Mfalme Solomoni alivyotengeneza vilikuwa vingi sana kwamba uzito wa shaba haukuweza kuonyeshwa.

19 Solomoni pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mungu:

madhabahu ya dhahabu;

meza za kuweka mikate Mitakatifu;

20 vinara vya taa vya dhahabu safi pamoja na taa zake ili ziwake mbele ya mahali pa ndani pa mahali Patakatifu kama ilivyoelekezwa;

21 maua ya dhahabu yaliyofanyizwa, taa na makoleo (vilikuwa vya dhahabu bora kabisa);

22 mikasi ya dhahabu safi, mabakuli ya kunyunyizia, masinia na vyetezo; milango ya dhahabu ya Hekalu: yaani milango ya ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, na milango ya ukumbi mkuu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CH/4-1ec53461b6822a89bcf07cbc99b022b3.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

16 − 8 =