2 Wafalme 12

Yoashi Anakarabati Hekalu

1 Katika mwaka wa saba wa kutawala kwake Yehu, Yoashi alianza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka arobaini. Jina la mama yake aliitwa Sibia, kutoka Beer-Sheba.

2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Mungu miaka yote ambayo Yehoyada kuhani alikuwa akimwelekeza.

3 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa, watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.

4 Yoashi akawaambia makuhani, “Kusanyeni fedha zote ambazo zitaletwa kama sadaka takatifu kwenye Hekalu laBwana, yaani, fedha zilizokusanywa kama kodi, fedha zilizopokelewa kutokana na nadhiri za watu binafsi na fedha zilizoletwa kwa hiari hekaluni.

5 Kila kuhani na apokee fedha kutoka kwa mmoja wa watunza hazina, nazo zitumike kukarabati uharibifu wo wote unaoonekana katika Hekalu.”

6 Lakini ikawa kufikia mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Mfalme Yoashi, makuhani walikuwa bado hawajalikarabati Hekalu.

7 Kwa hiyo Mfalme Yoashi akamwita Yehoyada kuhani na makuhani wengine na akawauliza, “Kwa nini hamtengenezi uharibifu uliofanyika hekaluni? Msichukue fedha zaidi kutoka kwa watunza hazina wenu kwa ajili ya matumizi yenu, lakini kuanzia sasa ni lazima fedha yote itumike kwa ajili ya kukarabati Hekalu.”

8 Makuhani wakakubali kuwa hawatakusanya tena fedha kutoka kwa watu na kwamba hawatakarabati Hekalu wenyewe.

9 Yehoyada kuhani akachukua kisanduku na akatoboa tundu kwenye kifuniko chake. Akakiweka kando ya madhabahu upande wa kulia unapoingia hekaluni mwaBwana. Makuhani waliolinda ingilio wakaweka ndani ya kisanduku fedha zote ambazo zililetwa katika Hekalu laBwana.

10 Kila mara walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani ya kisanduku, mwandishi wa jumba la kifalme na Kuhani Mkuu walikuja, wakazihesabu fedha hizo zilizoletwa katika Hekalu laBwanana kuziweka katika mifuko.

11 Wakiisha kuthibitisha kiasi cha hizo fedha, waliwapa watu walioteuliwa kusimamia kazi katika Hekalu. Kwa fedha hizo, wakawalipa wale watu waliofanya kazi katika Hekalu laBwana: yaani, maseremala na wajenzi,

12 waashi na wakata mawe. Walinunua mbao na mawe ya kuchongwa kwa ajili ya ukarabati wa Hekalu laBwana, na kulipia gharama nyingine zote za kulitengeneza.

13 Fedha zilizoletwa kwenye Hekalu hazikutumiwa kutengenezea masinia ya fedha, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, tarumbeta wala vyombo vingine vyo vyote vya dhahabu au fedha kwa ajili ya Hekalu laBwana;

14 zililipwa kwa wafanyakazi, ambao walizitumia kwa kukarabati Hekalu.

15 Wao hawakudai kupewa hesabu ya fedha kutoka kwa wale waliowapa ili kuwalipa wafanyakazi, kwa sababu walifanya kwa uaminifu wote.

16 Fedha zilizopatikana kutokana na sadaka za hatia na sadaka za dhambi hazikuletwa katika Hekalu laBwana; zilikuwa mali ya makuhani.

17 Wakati huu Hazaeli mfalme wa Aramu akapanda kuishambulia Gathi na akaiteka. Kisha akageuka ili kuishambulia Yerusalemu.

18 Lakini Yoashi mfalme wa Yuda akavichukua vyombo vyote vitakatifu vilivyowekwa wakfu na baba zake, yaani Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia wafalme wa Yuda, zawadi ambazo yeye mwenyewe alikuwa ameziweka wakfu pamoja na dhahabu yote iliyokutwa katika hazina za Hekalu laBwanana katika jumba la kifalme, akazipeleka kwa Hazaeli mfalme wa Aramu, ambaye hatimaye aliondoka Yerusalemu.

19 Kwa matukio mengine ya utawala wa Yoashi na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda?

20 Maafisa wake wakafanya shauri baya dhidi yake, nao wakamwua huko Beth-Milo, kwenye barabara itelemkayo kuelekea Sila.

21 Maafisa waliomwua walikuwa Yozabadi mwana wa Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa Shomeri. Akafa na akazikwa pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi. Naye Amazia mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/12-0bf3d5d4bc12bdb60a8e0c4ae1a28110.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × 2 =