2 Wafalme 14

Amazia Mfalme Wa Yuda

1 Katika mwaka wa pili wa kutawala kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.

2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipokuwa mfalme, naye akatawala katika Yerusalemu miaka ishirini na tisa. Jina la mama yake aliitwa Yehoadani, kutoka Yerusalemu.

3 Akatenda yaliyo mema machoni paBwana, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake.

4 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia miungu hapakuondolewa; watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.

5 Baada ya ufalme kuwa imara mikononi mwake, aliwaua wale maafisa waliomwua Mfalme Yoashi baba yake.

6 Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika kitabu cha Sheria ya Mose ambakoBwanaaliagiza akisema, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya baba zao, kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”

7 Yeye ndiye aliyewashinda Waedomu 10,000 katika Bonde la Chumvi na akauteka Sela katika vita akauita Yokitheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo.

8 Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tuonane uso kwa uso.”

9 Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda, akisema: “Mbaruti ulioko Lebanoni uliutumia ujumbe mwerezi ulioko Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni katika Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti chini ya nyayo zake.

10 Hakika umeishinda Edomu na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani! Kwa nini unachokoza nawe usababishe anguko lako mwenyewe na lile la Yuda pia?”

11 Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia, yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda.

12 Yuda ikashindwa na Israeli na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake.

13 Yehoashi mfalme wa Israeli akamkamata Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuvunja ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Kwenye Pembe, kisehemu chenye urefu wa kama dhiraa 400.

14 Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu laBwanana katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na kurudi Samaria.

15 Matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli?

16 Yehoashi akalala pamoja na baba zake na akazikwa Samaria pamoja na wafalme wa Israeli, naye Yeroboamu mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

17 Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli.

18 Matukio mengine ya utawala wa Amazia, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda?

19 Wakafanya shauri baya dhidi ya Amazia huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi nao wakamwua huko.

20 Akarudishwa kwa farasi na akazikwa huko Yerusalemu pamoja na baba zake, katika Mji wa Daudi.

21 Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azariaaliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita na kumfanya mfalme mahali pa baba yake Amazia.

22 Yeye ndiye aliyeijenga tena Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala pamoja na baba zake.

Yeroboamu Wa Pili Mfalme Wa Israeli

23 Katika mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, naye akatawala kwa miaka arobaini na mmoja.

24 Akafanya maovu machoni paBwanana hakuacha dhambi hata moja ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda.

25 Yeye ndiye aliyerudishia mipaka ya Israeli kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bahari ya Araba, sawasawa na neno laBwana, Mungu wa Israeli, lililosemwa kupitia mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii kutoka Gath-Heferi.

26 Bwanaalikuwa ameona jinsi kila mmoja katika Israeli, awe mtumwa au aliye huru alivyoteseka kwa uchungu; hapakuwepo na ye yote wa kuwasaidia.

27 Kwa kuwaBwanaalikuwa hajasema kuwa atafuta jina la Israeli chini ya mbingu, akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.

28 Kwa matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, yote aliyoyafanya na mafanikio yake ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na jinsi alivyorudisha Dameski na Hamathi kwa Israeli, ambayo ilikuwa mali ya Yaudi, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli?

29 Yeroboamu akalala pamoja na baba zake, wafalme wa Israeli. Naye Zekaria mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/14-7629f10205fbb5f2b98752a2a7631875.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 + 10 =