2 Wafalme 15

Azaria Mfalme Wa Yuda

1 Katika mwaka wa ishirini na saba wa kutawala kwake Yeroboamu mfalme wa Israeli Azaria mwana wa Amazia mfalme wa Yuda alianza kutawala.

2 Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili. Jina la mama yake aliitwa Yekolia kutoka Yerusalemu.

3 Akatenda yaliyo mema machoni paBwana, kama Amazia baba yake alivyofanya.

4 Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia miungu hapakuondolewa; watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.

5 Bwanaakampiga mfalme kwa ukoma mpaka siku aliyokufa, naye aliishi katika nyumba iliyotengwa peke yake. Yothamu mwana wa mfalme akawa msimamizi wa jumba la kifalme na akawatawala watu wa nchi.

6 Matukio mengine ya utawala wa Azaria na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda?

7 Azaria akalala pamoja na baba zake naye akazikwa karibu nao katika Mji wa Daudi, na Yothamu mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Zekaria Mfalme Wa Israeli

8 Katika mwaka wa thelathini na nane wa kutawala kwake Azaria mfalme wa Yuda, Zekaria mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miezi sita.

9 Akafanya maovu machoni paBwana, kama baba zake walivyofanya. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.

10 Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya shauri baya dhidi ya Zekaria. Akamshambulia mbele ya watu, akamwua na kuingia mahali pake kuwa mfalme.

11 Matukio mengine ya utawala wa Zekaria yameandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli.

12 Kwa hiyo neno laBwanalililonenwa kwa Yehu likatimia kwamba, “Uzao wako utaketi juu ya kiti cha enzi cha Israeli mpaka kizazi cha nne.”

Shalumu Mfalme Wa Israeli

13 Shalumu mwana wa Yabeshi akawa mfalme katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda, naye akatawala katika Samaria kwa mwezi mmoja.

14 Kisha Menahemu mwana wa Gadi akaenda kutoka Tirza mpaka Samaria. Akamshambulia Shalumu mwana Yabeshi huko Samaria, akamwua na kuingia mahali pake kuwa mfalme.

15 Matukio mengine ya utawala wa Shalumu na mauaji aliyoyafanya, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli.

16 Wakati ule, akianzia Tirza, Menahemu akashambulia Tifsa na kila mtu ndani yake na wale waliokuwa jirani kwa sababu walikataa kufungua malango yao. Akaiangamiza Tifsa yote na kuwapasua matumbo wanawake wote wenye mimba.

Menahemu Mfalme Wa Israeli

17 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa kutawala kwake Azaria mfalme wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi akawa mfalme wa Israeli na alitawala huko Samaria kwa miaka kumi.

18 Akatenda maovu machoni paBwana. Katika wakati wa utawala wake wote hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.

19 Kisha Pulu mfalme wa Ashuru akaishambulia Israeli. Menahemu mfalme wa Israeli akampa talanta 1,000 za fedhaili amsaidie na kumwezesha katika utawala wake.

20 Menahemu akatoza fedha hizi kwa nguvu kutoka kwa Israeli. Kila mtu tajiri alilazimika kuchanga shekeli hamsini za fedhaambazo alipewa mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akajiondoa na hakuendelea kuikalia nchi.

21 Matukio mengine ya utawala wa Menahemu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli?

22 Menahemu akalala pamoja na baba zake. Naye Pekahia mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Pekahia Mfalme Wa Israeli

23 Katika mwaka wa hamsini wa kutawala kwake Azaria mfalme wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, akatawala miaka miwili.

24 Pekahia akafanya uovu machoni paBwana. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.

25 Mmoja wa maafisa wake wakuu, Peka mwana wa Remalia, akafanya shauri baya dhidi yake. Akachukua watu hamsini wa Gileadi pamoja naye, akamwua Pekahia, pamoja na Argobu na Aria, katika ngome ya jumba la kifalme huko Samaria. Kwa hiyo Peka akamwua Pekahia, naye akaingia mahali pake kuwa mfalme.

26 Matukio mengine ya utawala wa Pekahia na yote aliyoyafanya yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli.

Peka Mfalme Wa Israeli

27 Katika mwaka wa hamsini na mbili wa kutawala kwake Azaria mfalme wa Yuda, Peka mwana wa Remalia akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, naye alitawala miaka ishirini.

28 Akafanya maovu machoni paBwana. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.

29 Wakati wa utawala wa Peka mfalme wa Israeli, Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru alikuja na kuiteka Iyoni, Abeli-Beth-Maaka, Yanoa, Kedeshi na Hazori. Akateka miji ya Gileadi na Galilaya, pamoja na nchi yote ya Naftali na kuwahamishia watu wote Ashuru.

30 Kisha Hoshea mwana wa Ela akafanya shauri baya dhidi ya Peka mwana wa Remalia. Akamshambulia na kumwua, kisha akaingia mahali pake kuwa mfalme katika mwaka wa ishirini wa Yothamu mwana wa Uzia.

31 Matukio mengine ya utawala wa Peka na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli?

Yothamu Mfalme Wa Yuda

32 Katika mwaka wa pili wa kutawala kwake Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli, Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala.

33 Alikuwa na miaka ishirini na mitano wakati alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Jina la mama yake aliitwa Yerusha binti Zadoki.

34 Akafanya yaliyo mema machoni paBwana, kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya.

35 Hata hivyo, mahali pa juu hapakuondolewa; watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu laBwana.

36 Matukio mengine ya utawala wa Yothamu na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda?

37 (Katika siku hizoBwanaakaanza kuwatuma Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia dhidi ya Yuda.)

38 Yothamu akalala na baba zake na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi, mji wa baba zake. Naye Ahazi mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/15-0c8f39f460884ddfc1a8935f6bc23374.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eight + 9 =