2 Wafalme 19

Hezekia Autafuta Msaada Wa Bwana

1 Wakati Mfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa nguo ya gunia, naye akaenda katika Hekalu laBwana.

2 Akamtuma Eliyakimu msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna mwandishi na makuhani viongozi, wote wakiwa wamevaa nguo ya gunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi.

3 Wakamwambia, “Hivi ndivyo asemavyo Hezekia: Siku hii ni siku ya huzuni, kukemewa na fedheha, kama vile wakati watoto wanapofikia hatua ya kuzaliwa lakini hakuna nguvu ya kuwazaa.

4 Inawezekana kuwaBwanaMungu wako atasikia maneno yote ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai na kwamba atamkemea kwa maneno ambayoBwanaMungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wanaishi.”

5 Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya,

6 Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hivi ndivyo asemavyoBwana: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenikufuru mimi.

7 Sikia! Ninakwenda kuweka roho ndani yake ambayo wakati atakaposikia habari fulani, atarudi kwenye nchi yake mwenyewe na huko nitahakikisha ameanguka kwa upanga.’ ”

8 Yule jemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alijiondoa na kumkuta mfalme akipigana dhidi ya Libna.

9 Mfalme Senakeribu alipokea taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, ametoka ili kupigana dhidi yake. Basi akatuma tena wajumbe kwa Hezekia wakiwa na neno hili:

10 “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usiruhusu huyo Mungu unayemtumaini akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’

11 Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wamefanya kwa nchi zote, walivyoziangamiza kabisa. Je, unafikiri wewe utaokoka?

12 Je, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa, yaani: miungu ya Gozani, Harani, Resefu na watu wa Edeni ambao walikuwa Telasari?

13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au Iva?”

Maombi Ya Hezekia

14 Hezekia akapokea barua kutoka kwa wajumbe naye akaisoma. Kisha akapanda kwenda katika Hekalu laBwanana kuikunjua mbele zaBwana.

15 Naye Hezekia akamwombaBwanaakisema: “EeBwana, Mungu wa Israeli, uliyeketi kwenye kiti chako cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako, ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe ndiye uliyeumba mbingu na dunia.

16 Tega sikio, EeBwana, usikie; fungua macho yako, EeBwana, uone; sikiliza maneno ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.

17 “Ni kweli, EeBwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya na nchi zao.

18 Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu bali ni miti na mawe tu, iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

19 Sasa basi, EeBwanaMungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili kwamba falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, EeBwana, ndiwe Mungu.”

Isaya Anatoa Unabii Kuanguka Kwa Senakeribu

20 Kisha Isaya mwana wa Amozi akatuma ujumbe kwa Hezekia kusema: “Hivi ndivyo asemavyoBwana, Mungu wa Israeli: Nimesikia maombi yako kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru.

21 Hili ndilo neno ambaloBwanaamelisema dhidi yake:

“ ‘Bikira Binti Sayuni

anakudharau wewe na kukudhihaki.

Binti Yerusalemu

anatikisa kichwa chake unapokimbia.

22 Unafikiri ni nani uliyemtukana na kumkufuru?

Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake

na kumwinulia macho yako kwa kiburi?

Ni dhidi ya yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!

23 Kupitia kwa wajumbe wako

umelundika matukano juu ya Bwana.

Nawe umesema,

“Kwa magari yangu mengi ya vita,

nimepanda juu ya vilele vya milima,

vilele vya juu sana katika Lebanoni.

Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu,

misunobari yake mizuri;

nimefikia sehemu zake zilizo mbali sana,

misitu yake iliyo mizuri sana.

24 Nimechimba visima katika nchi za kigeni

na kunywa maji yake.

Kwa nyayo za miguu yangu

nimekausha chemchemi zote za Misri.”

25 “ ‘Je, hujasikia?

Zamani sana niliamuru hili.

Siku za kale nilipanga hili;

sasa nimelifanya litokee,

kwamba umegeuza miji yenye ngome

kuwa lundo la mawe.

26 Watu wake, wakiwa wameishiwa nguvu,

wamevunjika moyo na wameaibishwa.

Wamekuwa kama mimea katika shamba,

kama machipukizi mabichi mororo,

kama majani yanayochipua kwenye paa la nyumba,

yaliyokauka kabla hayajakua.

27 “ ‘Lakini mimi ninajua ukaapo,

kuingia kwako na kutoka kwako

na jinsi unavyonighadhabikia.

28 Kwa sababu unaghadhabika dhidi yangu

na kiburi chako kimefika masikioni mwangu,

nitaweka ndoana yangu puani mwako

na lijamu yangu kinywani mwako

nami nitakufanya urudi

kwa njia ile uliyoijia.’

29 “Hii itakuwa ishara kwako, Ee Hezekia:

“Mwaka huu, utakula kile kinachoota chenyewe

na mwaka wa pili, utakula maotea yake.

Lakini katika mwaka wa tatu panda na uvune,

panda mashamba ya mizabibu

na kula matunda yake.

30 Kwa mara nyingine tena wale waliobaki wa nyumba ya Yuda

watatia mizizi chini na kuzaa matunda juu.

31 Kwa maana kutoka Yerusalemu watakuja mabaki,

na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika.

Wivu waBwanaMwenye Nguvu Zote ndio utakaotimiliza hili.

32 “Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyoBwanakuhusu mfalme wa Ashuru:

“Hataingia katika mji huu

wala kupiga mshale hapa.

Hatakuja mbele yake akiwa na ngao,

wala kuweka jeshi kuuzunguka.

33 Kwa njia ile aliyojia, atarudi;

hataingia katika mji huu,

asemaBwana.

34 Nitaulinda mji huu na kuuokoa,

kwa ajili yangu na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu.”

35 Usiku ule, malaika waBwanaakatokea na kuwaua watu 185,000 katika kambi ya Waashuru. Askari waliosalia walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali!

36 Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.

37 Siku moja, wakati alipokuwa anaabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamwua kwa upanga, nao wakatoroka kwenda katika nchi ya Ararati. Esar-Hadoni mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/19-27bb3072b84e788ebf4961ce6459df60.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

thirteen − 4 =