2 Wafalme 20

Ugonjwa Wa Hezekia

1 Katika siku zile, Hezekia akaugua na akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akamwendea na kusema, “Hivi ndivyoBwanaasemavyo: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”

2 Hezekia akaelekeza uso wake ukutani akamwombaBwanaakisema,

3 “EeBwana, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Hezekia akalia sana sana.

4 Kabla Isaya hajaondoka katika ua wa kati neno laBwanalikamjia:

5 “Rudi ukamwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, ‘Hivi ndivyoBwana, Mungu wa baba yako Daudi, asemavyo: Nimeyasikia maombi yako na kuona machozi yako; nitakuponya. Katika siku ya tatu kuanzia sasa utapanda kwenda Hekaluni mwaBwana.

6 Nitaongeza miaka kumi na tano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe na mji huu kutoka katika mkono wa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili yangu na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi!’ ”

7 Kisha Isaya akasema, “Tengeneza dawa ya kubandika itokanayo na tini.” Wakafanya hivyo na kuweka kwenye jipu, naye akapona.

8 Hezekia alikuwa amemwuliza Isaya, “Kutakuwa na ishara gani kwambaBwanaataniponya mimi na kwamba nitapanda Hekaluni mwaBwanasiku ya tatu tangu leo?”

9 Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara yaBwanakwako kwambaBwanaatafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”

10 Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”

11 Ndipo nabii Isaya akamwitaBwana, nayeBwanaakakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.

Wajumbe Kutoka Babeli

12 Wakati ule Merodaki-Baladani mwana wa Baladoni mfalme wa Babeli akamtumia Hezekia barua pamoja na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia.

13 Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonyesha vitu vyote vile vilivyokuwa katika ghala zake, yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu cho chote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.

14 Kisha nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumwuliza, “Hao watu wamesema nini na wametoka wapi?”

Hezekia akajibu, “Wametoka nchi ya mbali. Wametoka Babeli.”

15 Nabii akauliza, “Wameona nini katika jumba lako la kifalme?”

Hezekia akasema, “Wameona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”

16 Kisha Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno laBwana:

17 Hakika wakati utakuja ambao kila kitu katika jumba lako la kifalme na vyote vile ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii ya leo, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna cho chote kitakachobaki, asemaBwana.

18 Baadhi ya wazao wako, nyama yako mwenyewe na damu yako, ambao watazaliwa kwako, watachukuliwa, nao watakuwa matowashi ndani ya jumba la mfalme wa Babeli.”

19 Hezekia akajibu, “Neno laBwanaulilosema ni jema.” Mfalme alifikiri, “Lakini si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”

20 Matukio mengine ya utawala wa Hezekia, mafanikio yake yote na jinsi alivyotengeneza bwawa na mfereji ambao ulileta maji katika mji, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda?

21 Hezekia akafa akazikwa pamoja na baba zake. Manase mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/20-381dbdccacaf28d65462ca64941124b5.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

fourteen − 3 =