2 Wafalme 9

Yehu Atiwa Mafuta Kuwa Mfalme

1 Nabii Elisha akamwita mtu mmoja kutoka kwa wana wa manabii na kumwambia, “Jikaze viuno, ichukue hii chupa ya mafuta nenda Ramoth-Gileadi.

2 Ukifika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi. Mwendee, mtenge mbali na wenzake na umpeleke katika chumba cha ndani.

3 Kisha chukua hii chupa na umimine mafuta juu ya kichwa chake nawe utangaze, ‘Hivi ndivyo asemavyoBwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ Kisha ufungue mlango na ukimbie; usikawie!”

4 Basi yule kijana, ambaye ni nabii, akaenda Ramoth-Gileadi.

5 Wakati alipofika, akawakuta maafisa wa jeshi wameketi pamoja, akasema, “Nina ujumbe wako, ee jemadari.”

Yehu akauliza, “Kwa yupi mmoja wetu?”

Akamjibu, “Kwako wewe jemadari.”

6 Yehu akainuka na kuingia ndani ya nyumba. Ndipo yule nabii akamimina mafuta juu ya kichwa cha Yehu na kutangaza kwamba, “Hivi ndivyo asemavyoBwana, Mungu wa Israeli: ‘Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya watu waBwana, Mungu wa Israeli.

7 Inakupasa uiangamize nyumba ya bwana wako Ahabu, nami nitalipiza kisasi juu ya damu ya watumishi wangu manabii na damu ya watumishi wote waBwanailiyomwagwa na Yezebeli.

8 Nyumba yote ya Ahabu itaangamia. Nitamkatilia mbali kila mzaliwa wa kiume wa mwisho wa Ahabu katika Israeli, mtumwa ama aliye huru.

9 Nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama ile nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati na kama ile nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.

10 Kuhusu Yezebeli, mbwa watamla kwenye kiwanja huko Yezreeli na hakuna mtu atakayemzika.’ ” Kisha akafungua mlango na kukimbia.

11 Yehu alipotoka nje na kurudi kwenda kwa maafisa wenzake, mmoja wao akamwuliza, “Je, kila kitu ni salama? Kwa nini huyu mwenye wazimu alikuja kwako?”

Yehu akajibu, “Wewe unamfahamu huyo mtu na aina ya vitu ambavyo yeye husema.”

12 Wakasema, “Hiyo siyo kweli! Tuambie.”

Yehu akasema, “Haya ndiyo aliyoniambia: ‘Hivi ndivyo asemavyoBwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ ”

13 Wakaharakisha kuvua mavazi yao na kuyatandaza chini ya Yehu ili akanyage juu kwenye ngazi ya nje. Kisha wakapiga tarumbeta na kupiga kelele wakisema, “Yehu ni mfalme!”

Yehu Anamwua Yoramu Na Ahazia

14 Basi Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya shauri baya dhidi ya Yoramu. (Wakati huu, Yoramu na Israeli wote walikuwa wakiilinda Ramoth-Gileadi dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu,

15 lakini Mfalme Yoramu alikuwa amerudishwa Yezreeli ili kujiuguza kutokana na majeraha ambayo Waaramu walimtia katika vita na Hazaeli mfalme wa Aramu.) Yehu akasema, “Kama hii ndiyo nia yenu, msimruhusu hata mmoja kutoroka nje ya mji kwenda kupeleka habari huko Yezreeli.”

16 Ndipo akaingia katika gari lake la vita na kuendesha kwenda Yezreeli, kwa sababu Yoramu alikuwa amepumzika huko na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameshuka ili kumwona.

17 Mlinzi asimamaye juu ya kinara cha Yezreeli alipoona askari wa Yehu wanakuja, akaita akisema, “Naona askari wanakuja.”

Yoramu akaamuru, “Mtwae mpanda farasi umtume akakutane nao na kuuliza, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

18 Mpanda farasi akaondoka kwenda kukutana na Yehu na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme: ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

Yehu akamjibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”

Mlinzi akatoa habari, “Mjumbe amewafikia lakini harudi.”

19 Basi mfalme akamtuma mpanda farasi wa pili. Wakati alipowafikia akasema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

Yehu akajibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”

20 Yule mlinzi akatoa taarifa akasema, “Mjumbe amewafikia lakini hata yeye harudi. Uendeshaji ule ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi, anaendesha kama mwenye wazimu!”

21 Yoramu akaagiza, akasema, “Weka tayari gari langu la vita.” Na baada ya gari kuwa tayari, Yoramu mfalme wa Israeli na Ahazia mfalme wa Yuda wakaondoka, kila mmoja kwenye gari lake, ili kukutana na Yehu. Walikutana naye katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli.

22 Yoramu alipomwona Yehu akauliza, “Je, Yehu, umekuja kwa amani?”

Yehu akajibu, “Kunawezaje kuwa na amani wakati ibada za sanamu na uchawi wa mama yako Yezebeli ungaliko?”

23 Yoramu akageuka nyuma na kukimbia, akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini, Ahazia!”

24 Kisha Yehu akatwaa upinde wake na kumchoma Yoramu katikati ya mabega. Mshale ukapenya kwenye moyo wake naye akaanguka ghafula ndani ya gari lake.

25 Yehu akamwambia Bidkari, msaidizi wa gari lake, “Mwinue na umtupe katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. Kumbuka jinsi mimi na wewe tulivyokuwa tukiendesha pamoja magari yetu nyuma ya Ahabu baba yake wakatiBwanaalipotoa unabii huu kumhusu:

26 ‘Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya wanawe, nami kwa hakika nitakufanya uilipe juu ya shamba hili, asemaBwana.’ Sasa basi, mwinue na umtupe juu ya kiwanja kile, kulingana na neno laBwana.”

27 Wakati Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipiga kelele akisema, “Mwue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake kwenye njia ielekeayo Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido na akafia huko.

28 Watumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu na kumzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi.

29 (Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala katika Yuda).

Yezebeli Auawa

30 Kisha Yehu akaenda Yezreeli. Yezebeli aliposikia habari hii, akayapaka macho yake rangi, akatengeneza nywele zake na kutazama nje dirishani.

31 Yehu alipokuwa akiingia langoni, Yezebeli akasema, “Je, umekuja kwa amani, Zimri, wewe mwuaji wa bwana wako?”

32 Yehu akaangalia juu dirishani na kuita, “Je, ni nani aliye upande wangu? Ni nani?” Matowashi wawili au watatu wakamtazama.

33 Yehu akasema, “Mtupeni huyo mwanamke chini!” Kwa hiyo wakamtupa chini, sehemu ya damu yake ikatapanyika ukutani na nyingine juu ya farasi walipokuwa wakimkanyaga kwa miguu yao.

34 Yehu akaingia ndani akala na akanywa. Akasema, “Mshughulikieni huyo mwanamke aliyelaaniwa, mzikeni, kwa sababu alikuwa binti wa mfalme.”

35 Lakini walipotoka kwenda ili kumzika, hawakukuta kitu cho chote isipokuwa fuvu la kichwa, miguu yake na mikono.

36 Wakarudi na kumwambia Yehu, ambaye alisema, “Hili ndilo neno laBwanaalilosema kupitia kinywa cha mtumishi wake Eliya Mtishbi, kusema, Katika kiwanja cha Yezreeli mbwa wataila nyama ya Yezebeli.

37 Maiti ya Yezebeli itakuwa kama mavi shambani katika uwanja wa Yezreeli, kwamba hakutakuwepo mtu atakayeweza kusema, ‘Huyu ndiye Yezebeli.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2KI/9-fed5424eca56268f6c6cacbb1fa0f4e3.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × 4 =