2 Wakorintho 13

Maonyo Ya Mwisho

1 Hii ndiyo mara ya tatu nikija kwenu. “Shtaka lo lote lazima lithibitishwe na mashahidi wawili au watatu.”

2 Nimekwisha kuwaonya nilipokuwa pamoja nanyi mara ya pili. Sasa narudia wakati sipo, kwamba nikija tena sitawahurumia wale waliokuwa wametenda dhambi hapo awali na wengine wote,

3 kwa kuwa mnadai uthibitisho kwamba Kristo anazungumza kwa kunitumia mimi. Yeye si dhaifu katika kushughulika nanyi, bali ana nguvu katikati yenu.

4 Kwa kuwa alisulibiwa katika udhaifu, lakini anaishi kwa nguvu za Mungu. Vivyo hivyo, sisi tu dhaifu katika yeye, lakini katika kuwashughulikia ninyi tutaishi pamoja naye kwa nguvu za Mungu.

5 Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, hamtambui ya kuwa Yesu Kristo yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho!

6 Natumaini mtaona kuwa sisi hatukushindwa.

7 Lakini tunamwomba Mungu msije mkatenda kosa lo lote, si ili sisi tuonekane kuwa tumeshinda hilo jaribio, bali ili ninyi mtende lililo haki, hata kama tutaonekana kuwa tumeshindwa.

8 Kwa maana hatuwezi kufanya lo lote kinyume na kweli, bali kuithibitisha kweli tu.

9 Tunafurahi wakati wo wote sisi tunapokuwa dhaifu, lakini ninyi mkawa na nguvu. Nayo maombi yetu ni kwamba mpate kuwa wakamilifu.

10 Hii ndiyo sababu ninawaandikia mambo haya wakati sipo, ili nikija nisiwe mkali katika kutumia mamlaka yangu, mamlaka Bwana aliyonipa ya kuwajenga ninyi wala si ya kuwabomoa.

Salamu Za Mwisho

11 Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Iweni wakamilifu, mkafarijike, nieni pamoja, kaeni kwa amani, naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.

12 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu.

13 Watakatifu wote wanawasalimu.

14 Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2CO/13-22f9965197caab0b1b9f7bf9f1d3b32e.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × 4 =