1 Wakorintho 1

Salamu

1 Paulo, aliyeitwa kwa mapenzi ya Mungu kuwa mtume wa Yesu Kristo na Sosthene ndugu yetu.

2 Kwa Kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Kristo Yesu Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia:

3 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

Shukrani

4 Ninamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu kwa sababu ya neema yake mliyopewa katika Kristo Yesu.

5 Kwa kuwa katika Kristo mmetajirishwa kwa kila hali, katika kusema kwenu na katika maarifa yenu yote,

6 kwa sababu ushuhuda wetu kumhusu Yesu ulithibitishwa ndani yenu.

7 Kwa hiyo hamkupungukiwa na karama yo yote ya kiroho wakati mnangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

8 Yeye atawafanya imara mpaka mwisho, ili msiwe na hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo.

9 Mungu ni mwaminifu, ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Yesu Kristo, Bwana wetu.

Mgawanyiko Ndani Ya Kanisa

10 Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi.

11 Kwa maana ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi katikati yenu.

12 Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa”; na mwingine, “Mimi ni wa Kristo.”

13 Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulibishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?

14 Namshukuru Mungu kwamba sikumbatiza mtu ye yote miongoni mwenu isipokuwa Krispo na Gayo.

15 Kwa hiyo hakuna mtu ye yote miongoni mwenu anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa Jina langu.

16 (Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana. Lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine ye yote.)

17 Kwa maana Kristo hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili na nifanye hivyo si kwa kutumia maneno ya hekima ya kibinadamu ya kushawishi, ili msalaba wa Kristo usije ukakosa nguvu yake.

Kristo Hekima Na Nguvu Ya Mungu

18 Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.

19 Kwa maana imeandikwa:

“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima,

na kuzibatilisha akili za wenye akili.”

20 Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu?

21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale waaminio kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa.

22 Wayahudi wanataka miujiza na Wayunani wanatafuta hekima,

23 lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa, ambaye kwa Wayahudi ni kitu cha kukwaza na kwa Wayunani ni upuzi.

24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi pia Wayunani, Kristo ni nguvu na hekima ya Mungu.

25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na nguvu, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo.

27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili aviaibishe vyenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili aviaibishe vyenye nguvu.

28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko,

29 ili mtu ye yote asijisifu mbele za Mungu.

30 Mungu ndiye chanzo cha uzima wenu katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu na haki na utakaso na ukombozi,

31 ili kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/1-5f6dbac1c09057b91f50cfd908d59939.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

10 − 1 =