Amosi 6

Ole Kwa Wanaoridhika

1 Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni,

na ninyi mnaojisikia salama

juu ya Mlima Samaria,

ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine,

ambao watu wa Israeli wanawategemea!

2 Nendeni Kalne mkaone kutoka huko;

mwende hadi Hamathi iliyo kuu,

kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti.

Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili?

Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?

3 Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya

na kuleta karibu utawala wa kuogofya.

4 Ninyi mnalala juu ya vitanda

vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu

na kujinyosha juu ya viti vya fahari.

Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri

na ndama walionenepeshwa.

5 Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi

huku mkitunga nyimbo

za vinanda mbalimbali.

6 Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa

na mnajipaka mafuta mazuri,

lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yosefu.

7 Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza

kwenda uhamishoni;

karamu zenu na kustarehe kutakoma.

Bwana Anachukia Kiburi Cha Israeli

8 BwanaMwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe:BwanaMungu Mwenye Nguvu Zote asema:

“Nachukia kiburi cha Yakobo,

nachukia ngome zake;

nitautoa mji wao na kila kitu

kilichomo ndani mwake.”

9 Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa.

10 Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumwuliza ye yote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu ye yote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza kimya! Haturuhusiwi kutaja jina laBwana.”

11 Kwa kuwaBwanaameamuru,

naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande

na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.

12 Je, farasi waweza kukimbia kwenye miamba mikali?

Je, aweza mtu kulima huko kwa maksai?

Lakini mmegeuza haki kuwa sumu

na matunda ya uadilifu kuwa uchungu,

13 ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari

na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu

kwa nguvu zetu wenyewe?”

14 MaanaBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote asema,

“Nitainua taifa dhidi yenu,

Ee nyumba ya Israeli,

nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi

hadi Bonde la Araba.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/AMO/6-02314229646042210bd02661e6e1c8e8.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

14 − 10 =