Ayubu 29

Ayubu Anamaliza Utetezi wake

1 Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:

2 “Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita,

zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda,

3 wakati taa yake iliponiangazia juu ya kichwa changu

na kwa mwanga wake Mungu nikapita katikati ya giza!

4 Aha! Katika siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu,

wakati urafiki wa Mungu wa ndani

ulipoibariki nyumba yangu,

5 wakati Mwenyezi alipokuwa pamoja nami,

nao watoto wangu walipokuwa wamenizunguka,

6 wakati njia yangu ilipokuwa imenyweshewa siagi,

nao mwamba uliponimiminia vijito vya mafuta ya zeituni.

7 “Wakati nilipokwenda kwenye lango la mji

na kuketi katika kiwanja,

8 vijana waliniona wakakaa kando,

nao wazee walioketi wakasimama,

9 wakuu wakaacha kuzungumza

na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao,

10 wenye vyeo wakanyamazishwa,

nazo ndimi zao zikagandamana

na makaakaa ya vinywa vyao.

11 Ye yote aliyenisikia alinena mema juu yangu,

nao wale walioniona walinisifu,

12 kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada,

naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia.

13 Mtu aliyekuwa karibu na kufa alinibariki,

nami niliufanya moyo wa mjane kuimba.

14 Niliivaa haki kama vazi langu,

uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.

15 Nilikuwa macho ya kipofu

na miguu kwa kiwete.

16 Nilikuwa baba kwa mhitaji,

nilimtetea mgeni.

17 Niliyavunja meno makali ya waovu

na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao.

18 “Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe,

nazo siku zangu zitakuwa nyingi

kama chembechembe za mchanga.

19 Mizizi yangu itafika mpaka kwenye maji,

nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha.

20 Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu,

upinde wangu daima utaendelea

kuwa mpya mkononi mwangu.’

21 “Watu walinisikiliza kwa tumaini,

wakingojea ushauri wangu kwa utulivu.

22 Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi,

maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini.

23 Waliningojea kama manyunyu ya mvua

na kuyapokea maneno yangu

kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli.

24 Walipokata tamaa niliwaonyesha uso wa furaha,

nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao.

25 Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao;

niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake;

nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/29-6d71ac5ab2e4ddd690952a27673daf69.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty − 4 =