Ayubu 30

1 “Lakini sasa watu wadogo kwa umri

kuliko mimi wananidhihaki,

watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau

kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.

2 Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu,

kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?

3 Kukonda kwao kutokana na kupungukiwa na kwa njaa,

walizungukazunguka usiku katika nchi kame iliyo ukiwa,

isiyolimika wala kukaliwa na watu

4 Katika vichaka walikusanya mimea yenye ladha ya chumvi,

nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.

5 Walifukuzwa mbali na watu wao,

wakipigiwa kelele kama wevi.

6 Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka,

kwenye majabali na mahandaki.

7 Kwenye vichaka walilia kama punda

na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.

8 Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya,

waliofukuzwa watoke katika nchi.

9 “Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo,

nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.

10 Wananichukia sana na kujitenga nami,

wala hawasiti kunitemea mate usoni.

11 Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza

kamba ya upinde wangu na kunitesa,

wamekuwa huru kunitendea waonavyo.

12 Kuume kwangu kundi linashambulia;

huitegea miguu yangu tanzi,

hunizunguka kwa vita

wakiruka huko na huko kwa ukali dhidi yangu.

13 Huizuia njia yangu,

nao hufanikiwa katika kuniletea maafa,

nami sina ye yote wa kunisaidia.

14 Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana

katika ngome yangu;

katikati ya magofu huja na kunishambulia.

15 Vitisho vimenifunika;

heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo,

salama yangu imetoweka kama wingu.

16 “Sasa maisha yangu yamefikia mwisho,

siku za mateso zimenikamata.

17 Usiku mifupa yangu inachoma,

maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.

18 Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo,

hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.

19 Yeye amenitupa kwenye matope,

nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.

20 “EeBwana, ninakulilia wewe lakini hunijibu,

ninasimama, nawe unanitazama tu.

21 Wewe unanigeukia bila huruma,

unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.

22 Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo,

umenirusha huko na huko kwenye dhoruba kali.

23 Ninajua utanileta mpaka kifoni,

mahali ambapo wenye uhai wote wamewekewa.

24 “Hakika hakuna ye yote amshambuliaye mhitaji,

anapoomba msaada katika shida yake.

25 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?

Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?

26 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia,

nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.

27 Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii,

siku za mateso zinanikabili.

28 Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua,

ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.

29 Nimekuwa ndugu wa mbweha,

rafiki wa mabundi.

30 Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika,

mifupa yangu inaungua kwa homa.

31 Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo,

nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/30-d655d6bc17ce8e3ebf55bd52cfb01282.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eighteen + 5 =