Ayubu 3

Hotuba Ya Kwanza Ya Ayubu

1 Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake.

2 Akasema:

3 “Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali,

nao usiku ule iliposemekana,

‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’

4 Siku ile na iwe giza,

Mungu juu na asiiangalie,

nayo nuru isiiangazie.

5 Giza na kivuli kikuu kiikalie tena,

wingu na likae juu yake,

weusi na uifunike nuru yake.

6 Usiku ule na ushikwe na giza kuu,

usihesabiwe katika siku za mwaka,

wala usihesabiwe katika siku

za mwezi wo wote.

7 Usiku ule na uwe tasa,

sauti ya furaha na isisikike ndani yake.

8 Wale wazilaanio siku, wailaani hiyo siku,

wale walio tayari

# kumwamsha Lewiathani.

9 Nyota zake za alfajiri na ziwe giza,

nao ungojee mwanga bila mafanikio,

wala usiuone muonzi wa kwanza

wa mapambazuko,

10 kwa sababu huo usiku haukunifungia

mlango wa tumbo la mama yangu,

ili kuyaficha macho yangu

kutokana na taabu.

11 “Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa?

Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni?

12 Kwa nini pakawa na magoti ya kunipokea

na matiti ili nipate kunyonyeshwa?

13 Kwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani,

ningekuwa nimelala na kupumzika

14 pamoja na wafalme na washauri wa dunia,

waliojijengea kwa ajili yao mahali

ambapo sasa ni magofu,

15 pamoja na watawala waliokuwa na dhahabu,

waliozijaza nyumba zao kwa fedha.

16 Au kwa nini sikufichwa ardhini

kama mtoto aliyezaliwa mfu,

kama mtoto mchanga ambaye

kamwe hakuuona mwanga?

17 Huko waovu huacha kusumbua

na huko waliochoka hupumzika.

18 Wafungwa nao hufurahia utulivu wao,

hawasikii tena sauti ya kukemea

ya kiongozi wa watumwa.

19 Wadogo na wakubwa wamo humo,

na mtumwa ameachiwa huru

kutoka kwa bwana wake.

20 “Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni

na hao wenye uchungu kupewa uhai?

21 Kwa nini wale wanaotamani kufa hilo haliji,

wale watafutao kufa

zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa,

22 ambao hujawa na furaha

na shangwe wafikapo kaburini?

23 Kwa nini uhai hupewa mtu

ambaye njia yake imefichika,

ambaye Mungu amemzungushia boma?

24 Kwa maana kulia kwangu kwa uchungu

kwanijia badala ya chakula;

mlio wangu wa kusononeka

unamwagika kama maji.

25 Lile nililokuwa naliogopa limenijia;

lile nililokuwa ninalihofia limenipata.

26 Sina amani, wala utulivu;

sina pumziko, bali taabu tu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/3-2b7b03cbd95c9324befdebee068f04d2.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

3 × 5 =