Danieli 10

Maono Ya Danieli Kuhusu Mtu

1 Katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake Koreshi mfalme wa Uajemi, Danieli (ambaye aliitwa Belteshaza) alipewa ufunuo. Ujumbe wake ulikuwa kweli nao ulihusu vita vikubwa. Ufahamu wa ujumbe ulimjia katika maono.

2 Wakati huo, mimi Danieli, nikaomboleza kwa majuma matatu.

3 Sikula chakula kizuri, nyama wala divai havikugusa midomo yangu, nami sikujipaka mafuta kamwe mpaka majuma matatu yalipotimia.

4 Kwenye siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa nimesimama kwenye ukingo wa mto mkubwa Hidekeli,

5 nikatazama juu na mbele yangu alikuwapo mtu aliyevaa mavazi ya kitani na mshipi wa dhahabu safi kutoka ufazi kiunoni mwake.

6 Mwili wake ulikuwa kama kito cha zabarijadi safi, uso wake kama umeme wa radi, macho yake kama mwali wa moto, mikono yake na miguu yake kama mng’ao wa shaba iliyosuguliwa sana, nayo sauti yake kama ya umati mkubwa wa watu.

7 Mimi Danieli, nilikuwa ni mimi peke yangu niliyeona hayo maono, watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini waligubikwa na hofu kuu wakakimbia na kujificha.

8 Kwa hiyo niliachwa peke yangu, nikikodolea macho maono hayo makubwa, sikubakiwa na nguvu, rangi ya uso wangu ikabadilika kama aliyekufa, nikakosa nguvu.

9 Kisha nikamsikia akisema, nami nilipokuwa nikimsikiliza, nikalala kifudifudi nikapatwa na usingizi mzito.

10 Mkono ulinigusa, ukaninyanyua, nikapiga magoti na vitanga vyangu vikiwa vimeshika chini, huku nikiwa ningali bado ninatetemeka.

11 Akasema, “Danieli, wewe mtu upendwaye sana, fikiri kwa makini maneno ninayokwenda kunena nawe sasa, simama wima, kwa maana sasa nimetumwa kwako.” Naye aliposema nami haya, nikasimama nikitetemeka.

12 Ndipo akaendelea kusema, “Danieli usiogope. Tangu siku ya kwanza ulipotia moyo wako ili kupata ufahamu na kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja kwa ajili ya kuitikia maneno yako.

13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinizuia kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi.

14 Sasa nimekuja kukueleza mambo yatakayowatokea watu wako wakati ujao, kwa maana maono hayo yanahusu wakati ambao haujaja bado.”

15 Wakati alipokuwa akinieleza haya, nilisujudu uso wangu ukiwa umeelekea chini nikawa bubu.

16 Ndipo mmoja aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa midomo yangu, nami nikafungua kinywa changu, nikaanza kunena. Nikamwambia yule aliyesimama mbele yangu, “Nimepatwa na huzuni kubwa kwa sababu ya maono haya, bwana wangu, nimeishiwa nguvu.

17 Bwana wangu, mimi mtumishi wako nitawezaje kuzungumza na wewe? Nguvu zangu zimeniishia hata ninashindwa kupumua.”

18 Tena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu.

19 Akasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa, uwe na nguvu.”

Alipozungumza nami, nilipata nguvu nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.”

20 Kwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja,

21 lakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/DAN/10-8372668a01e90903cab32e79de2e87c7.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × four =