Ezekieli 27

Maombolezo Kwa Ajili Ya Tiro

1 Neno laBwanalikanijia kusema:

2 “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Tiro.

3 Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo:

“ ‘Ee Tiro, wewe umesema,

“Mimi ni mkamilifu katika uzuri.”

4 Mipaka yako ilikuwa katika moyo wa bahari,

wajenzi wako walikamilisha uzuri wako.

5 Walizifanya mbao zako zote

# kwa misonobari itokayo Seniri;

walichukua mierezi kutoka Lebanoni

kukutengenezea mlingoti.

6 Walichukua mialoni toka Bashani

wakakutengenezea makasia yako;

kwa miti ya msanduku

kutoka pwani ya Kitimu

wakatengeneza sitaha yako

na kuipamba kwa pembe za ndovu.

7 Kitani safi kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa tanga lako,

nacho kilikuwa bendera yako;

chandarua chako kilikuwa cha rangi ya buluu na ya zambarau

kutoka visiwa vya Elisha.

8 Watu kutoka Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia yako;

watu wako wenye ustadi, Ee Tiro,

walikuwa ndio mabaharia wako.

9 Wazee wa Gebalipamoja na mafundi stadi

walikuwa mafundi wako melini.

Meli zote za baharini na mabaharia wao

walikuja kwako ili kubadilishana bidhaa zako.

10 “ ‘Watu wa Uajemi, Ludi na Putu

walikuwa askari katika jeshi lako.

Walitundika ngao zao na chapeo zao kwenye kuta zako,

wakileta fahari yako.

11 Watu wa Arvadi na wa Heleki

walikuwa juu ya kuta zako pande zote;

watu wa Gamadi

walikuwa kwenye minara yako.

Walitundika ngao zao kuzizunguka kuta zako;

wakaukamilisha uzuri wako.

12 “ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali zako.

13 “ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki, walifanya biashara nawe, walibadilisha watumwa na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako.

14 “ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali zako.

15 “ ‘Watu wa Dedaniwalifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo.

16 “ ‘Watu wa Edomuwalifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, walibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe na akiki nyekundu.

17 “ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe, walibadilishana kwa ngano kutoka Minithi, mtama, asali, mafuta na marhamu ya kuponyeshea.

18 “ ‘Dameski, kwa sababu ya wingi wa kazi za mikono yako na ukuu wa utajiri wa mali, walifanya biashara nawe wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari.

19 “ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali, walikuletea mali za biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai.

20 “ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi.

21 “ ‘Arabia na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako waliobadilishana bidhaa zako na wana-kondoo, kondoo waume na mbuzi.

22 “ ‘Wafanya biashara wa Sheba na wa Rama walifanya biashara nawe, walibadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezi, vito vya thamani na dhahabu.

23 “ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe.

24 Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara.

25 “ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo

zinazokusafirishia bidhaa zako.

Umejazwa shehena kubwa

katika moyo wa bahari.

26 Wapiga makasia wako wanakupeleka

mpaka kwenye maji makavu.

Lakini upepo wa mashariki umekuvunja vipande vipande

katika moyo wa bahari.

27 Utajiri wako, bidhaa zako na mali zako,

mabaharia wako, manahodha wako,

mafundi wako wa meli,

wafanyabiashara wako na askari wako wote,

na kila mmoja aliyeko melini

atazama kwenye moyo wa bahari

siku ile ya kuvunjika kwa meli yako.

28 Nchi za pwani zitatetemeka

wakati mabaharia wako watakapopiga kelele.

29 Wote wapigao makasia

wataacha meli zao,

mabaharia wote na wanamaji wote

watasimama pwani.

30 Watapaza sauti zao

na kulia sana kwa ajili yako;

watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao

na kujivingirisha kwenye majivu.

31 Watanyoa nywele zao kwa ajili yako,

nao watavaa nguo za magunia.

Watakulilia kwa uchungu wa moyo

na kwa maombolezo makuu.

32 Watakapokuwa wanalia na kuomboleza juu yako,

watafanya maombolezo kukuhusu wakisema:

“Ni nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro,

katika moyo wa bahari?”

33 Wakati bidhaa zako zilipotoka baharini,

ulitosheleza mataifa mengi;

kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako

ulitajirisha wafalme wa dunia.

34 Sasa umevunjwavunjwa na bahari,

katika vilindi vya maji,

bidhaa zako na kundi lako lote

vimezama pamoja nawe.

35 Wote waishio katika nchi za pwani

wanakustaajabia;

wafalme wao wanatetemeka kwa hofu kuu,

nazo nyuso zao zimekunjamana kwa woga.

36 Wafanya biashara miongoni mwa mataifa wanakucheka;

umefikia mwisho wa kutisha

nawe hutakuwepo tena.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZK/27-5e0174060ef0a4ccecab004d567f1dce.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 + four =